Mataifa ya Ulaya kutuma chombo sayari ya Mars

ExoMars Haki miliki ya picha ESA
Image caption Chombo hicho kinapangiwa kutumwa mwaka 2021

Mawaziri wa utafiti kutoka bara Ulaya wanaokutana mjini Lucerne, Uswizi wamesisitiza kwamba mpango wa kutuma chombo maalum kinachoweza kusafiri kwenye sayari ya Mars mwaka 2021 bado utaendelea.

Wameahidi kutoa jumla ya euro €436m ambazo zinahitajika kufanikisha mpango huo.

Mradi huo umechelewa kiasi na unagharimu pesa zaidi kuliko ilivyotarajiwa, jambo lililoibua wasiwasi kwamba mataifa wanachama wa Shirika la Anga za Juu la Ulaya (ESA) huenda wakaufuta mpango huo.

Lakini mawaziri hao wamesema bado wamejitolea kuufanikisha.

Wamesema ushiriki wa nchi za Ulaya katika Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu (ISS) unafaa kuendelea hadi angalau 2024, na kuiwezesha ESA kufikia washirika wengine katika kituo hicho kinachoizunguka dunia - Marekani, Urusi, Japan na Canada.

Hilo litatoa fursa mpya kwa wana anga kutoka Ulaya kutembelea kituo hicho.

Kwenye mkutano huo wa mawaziri, imetangazwa kwamba Mwitaliano Luca Parmitano amependekezwa kuzuru kituo hicho 2019.

Mkutano huo wa mawaziri uliitishwa kujadili sera, miradi na ufadhili wa ESA kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mitano ijayo.

Mawaziri hao kutoka nchi 22 waliidhinisha kutumiwa kwa €10.3bn.

"Hiki ni kiasi kikubwa cha pesa na kitatuwezesha kupiga hatua mbele," Prof Jan Woerner, mkurugenzi mkuu wa ESA amesema.

Mpango huo wa kutuma chombo kinachoweza kutembea kwenye sayari ya Mars ni hatua ya pili ya mradi wa ExoMars, ambao unaendeshwa kwa ushirikiano na Urusi lengo kuu lilikiwa kubaini iwapo kuna uhai kwenye sayari hiyo.

Hatua ya kwanza ilihusisha kutumwa kwa setilaiti Mars kuchunguza gesi kwenye anga ya sayari hiyo kubaini iwapo kuna gesi inayotoka kutoka kwenye viumbe hai kwenye sayari hiyo.

Kwenye hatua ya pili, kutatumwa chombo kinachoweza safiri kwenye sayari hiyo kikiwa na roboti ambacho kitachimba na kufanya uchunguzi moja kwa moja.

Haki miliki ya picha ESA
Image caption Shirika la Anga za Juu la Ulaya huwa na mataifa wanachama 22
Haki miliki ya picha ESA/NASA
Image caption Mwitaliano Luca Parmitano huenda akarejea Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu

Jonathan.Amos-INTERNET@bbc.co.uk and follow me on Twitter: @BBCAmos

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii