Marekani yatuliza China juu ya Taiwan

Viongozi hao wamewasiliana kwa njiya ya simu Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais mteule wa Marekani Donald Trump na Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen

Ikulu ya Marekani imewasiliana na China na kuondoa wasi wasi uliozuka baada ya Rais Mteule Donald Trump kumpigia simu Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen.

Mazungumzo hayo ya wiki iliyopita yamezua wasi wasi kwani Marekani haina uhusiano wowote na Taiwan, ambayo China huchukulia kama Mkoa wake. Mamlaka za Beijing zimelalamikia vikali hatua hiyo. Afisa wa ikulu ya Marekani amesema wamesisitiza kutambua sera ya China moja.

Donald Trump ametetea hatua yake na kusema ilikua ni ngumzo la kawaida. Aidha Trump ametumia Mtandao wa Twitter kukosoa vikali sera za china kuhusu sarafu yake na operesheni zake katika Bahari ya 'South China Sea'.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Josh Earnest amesema kwamba sera ya Marekani kuhusu Taiwan imekuwepo kwa miongo minne sasa, na kwamba imeweka zaidi juhudi za kuimarisha usalama na uthabiti wa eneo hilo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen kwenye simu na Donald Trump

China ambayo Taiwan ni mmoja ya mikoa yake imetishia kutumia nguvu za kijeshi endapo kisiwa hicho kitajitangazia uhuru wake. Japo Marekani haitambui Taiwan kama taifa huru, pande mbili zina uhusiano wa karibu na vile vile Marekani haitambui umiliki wa China kwa Taiwan.

Kwa upande wake msemaji wa wizara ya kigeni ya China Lu Kang amesema uhusiano kati ya Marekani na China ni wa kuheshimiana. Gazeti moja la 'China Daily', limenadi kwenye ukurasa wake wa uhariri kwamba uchochezi wowote wa kuzua malumbano na tofauti kati ya Marekani na China haiwezi kusaidia kuifanya Marekani kuwa taifa bora duniani.