Kampuni ya Amazon imesema ina mpango wa kufungua duka la mboga litakalo tumia App

Haki miliki ya picha AMAZON

Kampuni ya Amazon imesema inampango wa kufungua duka la mboga na matunda ambapo mteja hatahitajika kulipa pesa taslim.

Kampuni hiyo inasema kuwa wateja wake wataweza kulipia bidhaa hizo kupitia App kwa jina Go.

Kampuni hiyo itatumia mfumo kama ule wa magari yasiokuwa na madereva.

Mfumo huo utakuwa na uwezo wa kutambua iwapo mteja amechukua bidhaa fulani au ameirejesha kwenye kabati na itakuwa na uwezo wa kudhibithi kikapu cha kuweka bidhaa hizo kupitia mfumo wa kiteknologia.

Mteja akiondoka katika duka hilo, akaunti yake ya Amazon inatozwa kulingana na bidhaa alizonunua na risiti inatumwa kwa mteja.

Duka la kwanza linatarajiwa kufungulia kwa umma huko Seattle nchini Marekani mapema mwakani.

Sekta ya ununuzi bidhaa za sokoni imefurika, na wateja wengi wanamatarajio mengi kutoka kwa kampuni hiyo ya Amazon, amesema Natalie Berg,mchambuzi wa Planet Retail.

Wateja watatumia kadi za kieletroniki katika duka hilo wakitumia App kwa jina Go. App hiyo itatumia teknologia ya komputa ili kuweza kudhibiti kile mteja anachochukua kutoka kabati hizo.

Kampuni hiyo ya Amazon imetumia miaka minne kutengeneza duka hilo.

Duka hilo litatarajiwa kupika vyakula vya asubuhi, vya mchana na jioni na hata vitafunio ambavyo hutengenezwa kila siku na wapishi waliokatika sehemu hiyo na hata kwenye maduka ya mikate.

Duka hilo litauza bidhaa kama vile mkate , maziwa na viungo ambavyo vinaweza kutumika kupika chakula cha watu wawili.