Takriban 100 wauawa baada ya paa la kanisa kuporomoka Nigeria

Huwezi kusikiliza tena
Paa la jengo la kanisa liliporomoka

Taarifa kutoka maeneo ya kusini mashariki mwa Nigeria, zasema kuwa takriban watu 100 wameuwawa pale paa la jengo moja la kanisa kuporomoka katika mji wa Uyo.

Taarifa zasema kuwa, kuna watu wengi ambao wamekwama ndani ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka.

Ajali hiyo imetokea wakati mamia ya waumini walipokuwa wakihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa muasisi wa kanisa la Reigners Bible, Akan Weeks kama askofu.

Image caption Ajali hiyo imetokea wakati mamia ya waumini walipokuwa wakihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa muasisi wa kanisa

Ujenzi wa majengo ya Kanisa hilo ulikuwa bado ukiendelea, huku serikali ikitangaza kuwa itaanzisha uchunguzi kubaini ikiwa utaratibu wa ujenzi mwema ulikiukwa au la.

Wakati wa mkasa huo, gavana wa jimbo la Akwa Ibom, Udom Emmanuel, alihudhuria ibada hiyo, kwa pamoja na wanasiasa wa eneo hilo, ambao waliepuka ajali hiyo.