Trump asema sera ya 'China Moja' huenda ikabadilika

Donald Trump alimpongeza Tsai Ing-wen aliposhinda urais Taiwan Januari Haki miliki ya picha AP
Image caption Donald Trump alimpongeza Tsai Ing-wen aliposhinda urais Taiwan Januari

Rais Mteule wa Marekani Donald Trump ametilia shaka iwapo sera ya Marekani ya kuendelea kutambua China kama taifa moja itaendelea, hatua iliyozua ghadhabu kutoka kwa vyombo vya habari vya serikali nchini China.

Hilo limetokea siku chache baada yake kupokea simu kutoka kwa rais wa Taiwan, hatua iliyoifanya Beijing kuilalamikia rasmi Marekani Tsai Ing-wen.

Chini ya sera hiyo, Marekani ina uhusiano rasmi wa kidiplomasia na China badala ya visiwa vya Taiwan, ambavyo China hutazama kama mkoa uliojitenga.

Sera hiyo imekuwa nguzo muhimu katika uhusiano kati ya Marekani na Uchina kwa miongo mingi.

Lakini Bw Trump amesema haoni sababu ya kuendelea na sera hiyo pia Beijing kulegeza baadhi ya mambo kwenye msimamo wake.

Akihojiwa na Fox News Jumapili, Bw Trump alisema: "Sioni ni kwa nini tunaendelea kufungwa na sera ya China Moja, hili linaweza tu kuendelea iwapo tutashauriana na China kuhusu mambo mengine, yakiwemo biashara."

Bw Trump pia alisema China haishirikiani na Marekani katika kushughulikia sarafu yake, kuhusu Korea Kaskazini au mzozo bahari ya Kusini mwa China.

Hakuna rais wa Marekani au rais mteule wa Marekani aliyewahi kuzungumza moja kwa moja na rais wa Taiwan.

Lakini akihojiwa na Fox, Bw Trump alisema Beijing haiwezi kuamua iwapo atapokea simu au la kutoka kwa kiongozi huyo wa Taiwan.

"Sitaki China wanieleze nitafanya nini na hii ni simu niliyopigiwa. Ilikuwa simu nzuri sana. Na, mbona mataifa mengine yaweze kusema siwezi kupokea simu hiyo?

"Nafikiri, kusema kweli, ingekuwa ni kukosa heshima, kutoipokea simu hiyo."

Hatua ya Bw Trump imepokelewa kwa hamaki na vyombo vya habari vya serikali nchini China.

Gazeti la Global Times limeonya kuwa "Sera ya China Moja haiwezi kubadilishwa na kitu kingine".

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi majuzi alitaja mawasiliano ya simu kati ya Trump na Tsai kuwa "mtego" wa Taiwan

Marekani ilivunja uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Taiwan mwaka 1979 na badala yake ikatambua eneo hilo kama sehemu ya China.

Ingawa uhusiano huo ulivunjwa, Marekani imeendelea na ushirikiano usio rasmi na Taiwan kwa miaka mingi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii