Chapecoense: Aliyenusurika asimulia yaliyojiri

Ndege hiyo ya LaMia ilianguka karibu na mji wa Medellin, Colombia mnamo 28 Novemba Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ndege hiyo ya LaMia ilianguka karibu na mji wa Medellin, Colombia mnamo 28 Novemba

Manusura wa ajali ya ndege iliyotokea nchini Colombia wiki mbili zilizopita na kuua wachezaji wa klabu ya Chapecoense ya Brazil amesema abiria hawakufahamishwa yaliyokuwa yakijiri kabla ya ndege hiyo kuanguka.

Watu 71 walifariki kwenye ajali hiyo, wengi wao wachezaji na maafisa wa klabu ya Chapecoense.

Rafael Henzel, 43, mwanahabari aliyekuwa ameandamana na klabu ya Chapecoense kwenye ndege hiyo ya shirika la LaMia plane, anasema hakuonywa na wahudumu wa ndege kuhusu hatari iliyowakabili.

Anasema hata hawakushauriwa kufunga mikanda ya usalama.

Bw Henzel ni miongoni mwa watu sita walionusurika ajali hiyo ya 28 Novemba.

Wachunguzi wanaamini ndege hiyo ilianguka baada ya kuishiwa na mafuta.

Akiongea kwenye mahojiano yake ya kwanza tangu ajali hiyo, Bw Henzel ameambia kituo cha televisheni cha Fantastico TV cha Brazil kwamba hakukutolewa tahadhari yoyote kwa abiria.

"Hakuna mtu hata mmoja aliyetuambia tujifunge mikanda," alisema. "Kila wakati, tulipouliza tungewasili wakati gani, tulijibiwa 'dakika 10'."

"Kisha, taa zikazima na injini pia ikazima. Hilo lilitushtua kiasi, lakini hatukuonywa. Hatukujua nini kilikuwa kinaendelea," anasema.

Anakumbuka jinsi watu walikimbia na kurudi kwenye viti vyao kulipotokea giza baada ya taa kuzima.

Lakini anasema hakuna aliyetarajia ndege ingeanguka.

Kurejea nyumbani

Mwanahabari huyo ameelezea nyakati za mwisho kwenye ndege hiyo, ambapo alikuwa ameketi sehemu ya nyuma ya ndege kati ya mwanahabari Renan Agnolin na mpiga picha Djalma Araujo Neto.

Anasema wakati wa huzuni zaidi kwake ni wakati alipogundua kwamba wawili hao, waliokuwa ameketi nao walikuwa wamefariki.

Bw Henzel alivunjika bavu saba na alikuwa abiria wa mwisho kuokolewa.

Aliokolewa wakati ambapo matumaini ya kuwapata manusura yalikuwa yanafifia.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mashabiki wa soka Brazil wamekuwa wakitoa heshima zao kwa wachezaji waliofariki

Anasema aliona tochi za maafisa wa uokoaji na akawaita kwa sauti kuwajulisha alipokuwa na kwamba alikuwa hai.

Amesifu juhudi za maafisa wa uokoaji wa Colombia kwa kazi yao licha ya kwamba lilikuwa eneo la milimani lisilofikika kwa urahisi, kulikuwa na mvua na ilikuwa usiku.

Yeye, na raia wengine wawili wa Brazil walionusurika, wachezaji Jakson Follmann na Alan Ruschel, wanatarajiwa kusafirishwa kwa ndege kutoka Colombia hadi Brazil siku chache zijazo.

Mchezaji wa Chapecoense Neto bado yuko hai katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali moja Colombia.

Maafisa wa ndege kutoka Bolivia Ximena Sanchez na Erwin Tumiri tayari wamerejea kwao Bolivia.

Jumapili, klabu za soka Brazil zilitoa heshima kwa wachezaji 19 wa Chapecoense waliofariki katika ajali hiyo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii