Wafungwa wawili wa mauaji ya kimbari Rwanda waachiliwa huru

Serikali ya Rwanda haijafurahishwa na hatua hiyo
Image caption Serikali ya Rwanda haijafurahishwa na hatua hiyo

Mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda imewaachia huru wafungwa wawili wa mauaji ya kimbari kabla ya kumaliza vifungo vyao.

Ferdinand Nahimana na Padri Emmauel Rukundo walikuwa wamehukumiwa kufungwa jela miaka 30 na 23 mtawalia kwa makosa ya kutekeleza mauaji ya kimbari.

Wote walikuwa katika jela ya Koulikoro nchini Mali.

Mahakama imesema wamekamilisha theluthi mbili ya vifungo vyao na wamekuwa na mwenendo mzuri gerezani.

Sababu zilizotolewa na jaji Theodor Meron ambaye pia ni mkuu wa chombo kilichochukua mikoba ya mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda, ni kwamba japo watu hao walipatikana na hatia ya makosa makubwa waliweza kuonyesha mwendendo mzuri wakiwa gerezani na kwamba wamekamilisha theluthi mbili ya vifungo vyao.

Uamuzi huu haujapokelewa vyema na serikali ya Rwanda.

Msemaji wa ofisi ya mashtaka ya Rwanda Faustin Nkusi ameambia BBC kwa njia ya simu: „Hawa watu walikuwa miongoni mwa viongozi waliopanga na kutekeleza mauaji ya kimbari. Kweli ni utaratibu wa kisheria lakini haujatufurahisha kwa sababu kwanza hukumu waliyokuwa wamepewa ni ndogo ukilinganisha na mchango wao katika mauaji hayo, sasa leo unasema waachiwe huru eti walikuwa na mwendendo mzuri?"

Watu 10 tayari wamekwishaachiliwa huru na mahakama hiyo kabla ya kumaliza vifungo vyao miongoni mwa wafungwa 61 waliohukumiwa na mahakama hiyo kwa hatia ya mauaji ya kimbari.

Ferdinand Nahimana aliyekuwa mhadhiri wa chuo kikuu cha Rwanda aliyebobea katika masuala la historia.

Anafahamika sana nchini Rwanda kama mkuu wa zamani wa shirika la utangazaji la serikali na hasa hasa mwanzilishi wa Radio television des mille collines (RTLM) ambayo inatuhumiwa kuhamasisha Wahutu kuwaua Watutsi wakati wa mauaji ya kimbari.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii