Watanzania hutafuta nini mtandaoni?

Raia wakipigwa picha na picha za Hillary Clinton na Donald Trump ubalozi wa Marekani mjini Dar es Salaam, Tanzania mnamo Novemba 7, 2016.

Chanzo cha picha, AFP/GETTY

Kampuni ya Google imetoa ripoti ya mambo ambayo Watanzania walitafuta sana mtandaoni mwaka 2016.

Maelezo waliyotafuta yameangazia masuala ya afya, biashara na fedha na pia burudani.

Pia, yapo masuala ya kijamii.

Walichotafuta sana mtandaoni ni matokeo ya darasa la saba 2016, zikifuatwa na Beka Boy, mtandao wa burudani.

Walitafuta pia Mkekabet, ambao ni mtandao wa kuweka dau kuhusu matokeo ya mechi za kandanda na mashindano mengine ya kimichezo.

Walitafuta pia habari kuhusu matokeo ya kidato cha nne 2016, pamoja na Raymond, ambapo huenda labda walitaka habari na maelezo kumhusu mwanamuziki Rayvanny ambaye jina lake halisi ni Raymond. Kuna pia mwanamuziki Hekima Raymond mzaliwa wa Moshi, Tanzania.

Walitaka kujua kufanya nini?

Watanzania walitaka sana kujua jinsi ya kuweka tone la dawa jichoni, ikifuatwa na jinsi ya kuwapata wawekezaji na wafadhili.

Walitaka pia kujua sana jinsi ya kukuza nyusi na pia jinsi ya kujua mwanamke atajifungua tarehe gani.

Huenda kukoroma likawa tatizo linalowasumbua wengi kwani, kwenye nambari tano, Watanzania walitaka kujua jinsi ya kuacha kukoroma.

Kujua maana

Katika maneno ambayo Watanzania walitafuta sana maana, nambari tatu kuna neno la kushangaza 'Bae'.

Ni ufupisho wa neno 'Babe', mtoto au mpenzi kwa Kiingereza. Pia ni akronimi ya before anyone else, kabla ya wengine wote.

Kuna wimbo wa Sauti Sol na Alikiba kwa jina Unconditionally Bae, ambao huenda uliwafanya wengi kutaka kujua maana ya 'Bae'.

Mambo yaliyotafutwa sana Tanzania 2016:

 • matokeo ya darasa la saba 2016
 • beka boy
 • mkekabet
 • salehe jembe juni 26 2016
 • Malazi Arusha
 • euro 2016
 • matokeo ya kidato cha nne 2016
 • yinga media
 • muungwana
 • Raymond

Walichotaka kujua sana kufanya:

 • Jinsi ya kuweka tone la dawa jichoni
 • Jinsi ya kupata wawekezaji/wafadhili
 • Jinsi ya kukuza nyusi
 • Jinsi ya kujua tarehe ya kujifungua
 • Jinsi ya kuacha kukoroma
 • Jinsi ya kufanya cd kuweza kuifungulia kompyuta
 • Jinsi ya kuomba na ubani
 • Jinsi ya kupika danish na croissant
 • Jinsi ya kuanzisha kiwanda cha chokoleti
 • Jinsi ya kujua iwapo mtoto amegeuka

Ni nini:

 • Furaha kamili/upeo wa furaha ni nini
 • Malengo ni nini
 • Bae maana yake ni nini
 • Elimu rasmi ni nini
 • Ndoa ya wake wengi ni nini
 • Hesabu ya jumla ni nini
 • Matumizi ya pesa ni nini
 • Soko la kubadilishana sarafu za kigeni ni nini
 • Mfumo ni nini
 • Ghala ni nini