Waziri wa Nigeria atangazwa naibu katibu mkuu wa UN

Amina Mohammed ni waziri wa mazingira wa Nigeria Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Amina Mohammed ni waziri wa mazingira wa Nigeria

Anayetarajiwa kuchukua hatamu kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, amemtangaza Amina Mohammed kama naibu wake.

Guterres ametangaza uteuzi wa wanawake wengine wawili kwa nyadhifa za juu katika Umoja wa Mataifa.

Guterres ametoa tangazo hilo kupitia kwa msemaji wake Stephane Dujarric. Bi Amina Mohammed ni waziri wa mazingira wa Nigeria.

Alihudumu kama msaidizi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeondoka Ban Ki-Moon, kwenye ajenda ya maandeleo ya mwaka 2030.

Lakini serikali ya Nigeria bado haijasema kuwa imejulishwa kuhusu uteuzi huo.

Bwana Guterres aliseka siku ya Jumatatu baada ya kuapishwa kuwa suala la usawa wa jinsia litakuwa ajenda yake kuu kwenye Umoja wa Mataifa. Mkuu huyo mpya wa Umoja wa Mataifa ataingia ofisini Januari mosi mwaka 2017 kwa kipindi cha miaka mitano.