Zsa Zsa Gabor, mwigizaji aliyeolewa mara tisa

Zsa Zsa Gabor Haki miliki ya picha Rex Features

Mwigizaji mashuhuri Mmarekani Zsa Zsa Gabor amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 99.

Wengi wanasema nafasi kuu zaidi aliyoiigiza maishani ni kujiigiza mwenyewe na kugeuza maisha yake kuwa kama filamu moja ndefu.

Ingawa aliigiza kwenye zaidi ya filamu 70, ndoa zake nyingi na maisha yake ya kifahari ndivyo vilivyompatia sifa nyingi.

Alipokuwa katika jamii ya waigizaji Hollywood, alidumisha sifa fulani za kipekee na kujionyesha kama mtu wa familia tajiri yenye mamlaka Hungary.

Alizungumza lugha saba, lakini licha ya kuishi California zaidi ya nusu karne, hakuwahi kupoteza lafudhi yake.

Alizaliwa Sari Gabor mjini Budapest tarehe 6 Februari 1917 lakini mara moja alipewa jina la utani Zsa Zsa na watu wa familia yake.

Alikuwa binti wa pili wa baba mwanajeshi na mama tajiri wa vito.

Alitaka awali kuwa daktari wa upasuaji wa mifugo lakini mamake hakutaka hilo. Kutokana na urembo wake, alielekea njia tofauti - mitindo na uigizaji.

Mamake alikuwa Myahudi, ingawa binti zake watatu walikuwa waumini wa kanisa Katoliki. Huo ulikuwa uamuzi wa busara ikizingatiwa kwamba Hungary ilikuwa inatawaliwa na Miklos Horthy aliyekuwa na urafiki na Adolf Hitler wa Ujerumani.

Haki miliki ya picha Rex Features
Image caption Ndoa yake kwa George Sanders ilikuwa ya tatu

Akiwa safarini Vienna mwaka 1934, Gabor alitambuliwa na mwanamziki wa Austria Richard Tauber ambaye alimpa nafasi katika uigiaji wa wimbo jukwaani, mara yake ya kwanza kuigiza.

Urembo wake ulipelekea mwishowe kutawazwa kwake kuwa Miss Hungary mwaka 1936.

Lakini alipokonywa taji hilo baadaye baada ya kubainika alihadaa kuhusu umri wake ndipo aruhusiwe kushiriki.

Mwaka 1937, aliolewa na msomi kutoka Uturuki Burhan Asaf Belge.

Ndoa yao hata hivyo, ya kwanza kati ya tisa alizofunga, ilivunjika 1941.

Wazazi wake walikuwa wametalikiana na yeye na mamake wakahamia Marekani kujiunga na dadake, Eva.

Huko, urembo wake ulimuwezesha kupata nafasi katika uigizaji wa michezo ya kuigiza.

Filamu yake ya kwanza kuigiza ilikuwa ya 1952, filamu ya muziki kwa jina Lovely To Look At ya MGM, ingawa hakuigiza mistari yoyote ya Kiingereza.

Wakati huu, alikuwa tayari kwenye harusi yake ya tatu, kwa mwigizaji George Sanders, baada ya kutalikiana na mumewe wa pili, tajiri mmiliki wa mahoteli Conrad Hilton

Mwaka huo, alipata ufanisi mkubwa, alipoigiza katika filamu ya John Huston kwa jina Moulin Rouge. Mwelekezi huyo wa filamu baadaye alimweleza kama mwigizaji mzuri ajabu.

Image caption Akiwa katika studio za BBC TV mwaka 1952

Aliigiza katika filamu 14 zaidi miaka ya 1950, baadhi maarufu.

Moja ambayo baadaye iliishia kuwa mzigo kwake ni Queen of Outer Space, ambapo aliigiza kama kiumbe kutoka sayari ya Zuhura.

Baadaye alieleza filamu hiyo kama "filamu mbovu sana ambayo hukaa ikichipuka".

Lakini nafasi kuu zaidi aliyokuwa nayo maishani ni kuwa nyota wa Hollywood, wa familia ya Gabor na mke wa wanaume wengi.

Mamake wakati mmoja inadaiwa alimwambia: "Si lazima umuoe mwanamume yeyote unayefanya mapenzi naye."

Gabor alisema alikuwa anaoa kwa sababu hakuwahi "kuacha kuwa Mkatoliki moyoni."

Alifahamika kama mtu wa udaku, na mtu wa kujiingiza kwenye mahusiano mengi.

Baada ya kutalikiwa na George Sanders mwaka 1954, alikaa kwa muda bila kuigiza sasa akijijengea sifa kwama mtu maarufu wa Hollywood.

Haki miliki ya picha Rex Features
Image caption Filamu ya Moulin Rouge ilimzolea sifa

Aliolewa tena mwaka 1962 na Herbert Hutner, mhudumu wa benki ambaye alimzidi umri kwa miaka tisa.

Harusi yao ilidumu miaka minne.

Mwaka 1966 aliolewa na mume wake wa tano, Joshua S Cosden Jr, lakini ndoa yao ikavunjika baada ya miezi saba.

Alikaa miaka tisa kabla ya kufunga ndoa na mbunifu wa Barbie doll, Jack Ryan.

Ndoa yao ilipovunjika baada ya miezi 18 pekee, aliolewa mara moja na Michael O' Hara.

Wakati huu, ndoa yake ilidumu kwa muda - miaka saba.

Alihusisha na wanaume wengine kadha wakiwemo Sean Connery, Frank Sinatra na Richard Burton.

Harusi yake ya nane, kwa wakili raia wa Mexico Felipe de Alba - ambayo ilifanyika baharini - ilibatilishwa baadaye kwa sababu Gabor alisema boti halikuwa mbali sana na pwani kuifanya kuwa halali.

Alikuwa na bahati, kwani kimsingi alikuwa bado ameolewa na mume wake wa saba wakati huo.

Uhusiano wake uliojaa vituko zaidi ulikuwa na Porfirio Rubirosa. Alipomchagua mrithi mwingine badala ya Gabor, mwanamke huyo alitokea jukwaani Las Vegas akidai kuonyesha jeraha kwenye jicho alilosema alipata mikononi mwa Rubirosa.

Haki miliki ya picha Allied Artists
Image caption Hakupendezwa na filamu ya Queen of Outer Space

Alijua sana kujiuza na kujipendekeza na mwaka 1989, alijibizana na polisi Los Angeles na akapatikana na hatia ya kumshambulia afisa wa usalama.

Alifungwa siku tatu pekee.

Baadaye, alifanyia mzaha na kurejea kisa hicho katika filamu kama vile The Naked Gun 2 1/2: The Smell of Fear na The Beverly Hillbillies.

Mwishoni mwa maisha yake, alizoea sana kufika kortini.

Machi 2005, alilipa $2m kwenye kesi aliyoshtakiwa na dereva wa gari lililohusika kwenye ajali iliyomlemaza na kumwacha akitumia gari la magurudumu.

Miezi mitatu baada ya hapo, akiwa na mumewe wa mwisho, Frederic von Anhalt, alimshtaki binti yake wa pekee Francesca Hilton, akidaiwa kumtapeli mamake $2m za kununua nyumba mpya.

Hata hivyo, wakati huo alikuwa na miaka themanini na afya yake ilianza kudorora.

Alilazwa hospitalini mara kadha baada ya kuanza kuvimba miguuni na damu kuganda mwilini.

Alifanyiwa upasuaji.

Mwishowe, alikatwa mguu.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Harusi yake ya tisa ndiyo iliyodumu zaidi

Licha yake kupenda sana vito na wanaume, wanaume wote waliowahi kumuoa walisalia kumpenda.

Kwenye kitabu kuhusu maisha yake, George Sanders alisema watu walikosa kumuelewa vyema mke wake huyo wa zamani.

Gabor mwenyewe aliwahi kusema: "Wanawake Wamarekani ni wapenda mali sana. Hufunzwa tu jinsi ya kupata pesa kutoka kwa mwanamume.

"Wanawake wa Ulaya hutaka mwanamume wanayeweza kumpenda, kumpikia na kuwa mke mwema kwake."

Lakini wakati mmoja, akizungumzia upendo, ndoa na talaka, alisema wakati mmoja: "Sijawahi kumchukia mwanamume kiasi cha kufikiria kumrejeshea vito vyake vya almasi."

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii