Merkel ataka kufahamu zaidi kuhusu mshambulizi wa Berlin

Polisi wa Ujerumani wametoa picha za Anis Amri

Chanzo cha picha, BKA / HANDOUT

Maelezo ya picha,

Polisi wa Ujerumani wametoa picha za Anis Amri

Kiongozi wa Ujerumani, Angela Merkel, ameitisha taarifa kamili juu ya kesi inayomhusu Anis Amri, raia wa Tunisia aliyekuwa akitakikana nchini Ujerumani kwa kushambulia soko la Krismasi jijini Berlin.

Amri alipigwa risasi na kuuawa hiyo jana na polisi nchini Italia. Bethany Bell ametutumia taarifa ifuatayo kutoka Berlin.

Kuna hali ya utulivu nchini Ujerumani ambapo watu wametambua kuwa Anis Amri si hatari tena nchini humo.

Lakini kama anavyosema Angela Merkel, kesi hii inazusha maswali mengi sana. Maafisa wa Ujerumani wanasema kuwa wapelelezi wa tukio hilo wanataka kujua iwapo Amri alikuwa na mtandao wa wafuasi.

Watataka pia kujua kwa nini ilikuwa vigumu yeye kuondolewa nchini licha ya amri nyingi kutolewa na kwa nini maafisa wa usalama walikoma kumfuatilia licha ya kufahamu kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu na wanachama kadhaa wa Waislamu wenye itikadi kali.

Licha kutangazwa kuwa yeye alikuwa mshukiwa mkuu katika shambulio la Berlin, aliweza kusafiri kusafiri katika mataifa kadhaa ya Ulaya.

Bi Merkel alisema kuwa taifa lake litachukua hatua kambambe kuimarisha usalama. Yeye na Serikali yake wametiliwa shinikizo kutekeleza ahadi hiyo.