Gumzo la benchi, tiba ya magonjwa ya kiakili

Hospitali
Image caption Hospitali

Unaamini kuwa mazungumzo ya muda na daktari kwenye benchi inaweza kupunguza maradhi ya akili?

Kulingana na matokeo ya utafiti uliofanywa na Chuo kikuu cha Zimbabwe, Chuo cha London cha usafi na magonjwa ya nchi za joto, na taasisi ya King's mjini London, Wagonjwa wenye maradhi ya kiakili wamepata nafuu baada ya mazungumzo ya muda kwenye benchi.

Benchi ya urafiki inahusisha vikao sita vya ushauri vinavyodumu dakika 45 ambavyo vinaandaliwa katika dawati la mbao ndani ya mandhari ya hospitali.

Utafiti huo ulihusisha zaidi ya wagonjwa 550 waliohitimu umri wa miaka 18 au Zaidi wenye shinikizo ya akili.

Zaidi ya hospitali 20 mjini Harare zilitumika kufanya uchunguzi huo uliodumu miezi sita.

Matokeo yalionyesha kuwa, wagonjwa waliohudumiwa kwa njia ya benchi, walipunguza hatari za shinikizo ya akili kwa asilimia 72 wakilinganishwa na wagonjwa waliotibiwa kwa njia ya kawaida.

Matatizo ya kiakili yamekuwa yakiathiri mataifa yenye mapato madogo na kuwapa mzigo wa kutoa huduma za matibabu.

Aidha mataifa mengi yana uhaba wa wataalam wa kiakili wa kuwasaidia wagonjwa hao. Taifa la Zimbabwe limeathirika Zaidi kwani Zaidi ya asilimia 25 ya raia wa taifa hilo, wanaosaka matibabu wana shinikizo ya akili.

"Zimbabwe ina pengo kubwa kukabiliana na matatizo ya kiakili, Wataalam 12 pekee wa afya ya akili wanawahudumia Zaidi ya watu milioni 13.Benchi ya urafiki inatoa fursa ya kuziba huu ufa na kuleta mabadiliko kwa maisha ya watu wanaougua matatizo ya kiakili."

Mwanzilishi wa mpango huo, Daktari Dixon Chibanda, kutoka chuo kikuu cha Zimbabwe amesema,

Kwa sasa wataalam hao wanapendekeza kufanya majaribio hayo yatekelezwa katika mataifa mengine matatu barani Afrika.