Wafungwa wengi watoroka jela kusini mwa Ufilipino

Kundi la MILF lilitia saini mkataba wa kusitisha mapigano majuzi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kundi la MILF lilitia saini mkataba wa kusitisha mapigano majuzi

Watu kadha wenye silaha wameshambulia jela moja kusini mwa Ufilipino na kuchangia kutoroka kwa zaidi ya wafungwa 150.

Washambuliaji hao wamemuua askari jela mmoja. Mfungwa mmoja alijeruhiwa

Maafisa wanashuku kuwa washambuliaji hao wana uhusiano na makundi ya Kiislamu yanayotaka kujitenga.

Ufilipino, taifa ambalo lina Wakatoliki wengi, limekuwa likikabiliana na makundi yanayopigania kujitenga kwa maeneo ya kusini kwa miongo mingi

Maeneo hayo hushuhudia visa vya utekaji nyara, ghasia na wafungwa kutoroka jela.

Kisa cha karibuni zaidi kilitokea katika Gereza la Wilaya ya Cotabato Kaskazini karibu na mji wa Kidapawan city, katika kisiwa cha Mindanao.

Maafisa wa magereza wanasema washambuliaji walifika mwenzo wa saa saba usiku na kuanza kufyatua risasi katika gereza hilo lenye wafungwa zaidi ya 1,500.

Ufyatulianaji wa risasi ulidumu kwa karibu saa mbili.

Katika mtafaruku uliotokea, baadhi ya wafungwa walikimbilia eneo la nyuma ya gereza na kuruka ua kwa kurundika vitanda vyao na kuvitumia kama ngazi, kituo cha habari cha GMA News kimesema.

Wanajeshi na maafisa wa polisi wanawasaka wafungwa waliotoroka.

Wafungwa sita kufikia sasa wamekamatwa tena.

Makundi ya Kiislamu kama vile Moro Islamic Liberation Front (MILF) na Abu Sayyaf yamekuwa wakitekeleza mashambulio ya kigaidi na kuwateka nyara watalii kwa muda mrefu.

MILF kwa sasa wanaendelea na mchakato wa amani kati yao na serikali.

Hata hivyo, kuna baadhi ya wapiganaji waliokataa mwafaka wa kusitisha mapigano.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii