Mapumziko ya siku moja kwa walio na hedhi yazua hisia Zambia

Ndekela Mazimba anasema kuwa siku hiyo inamsadia kukabiliana na uchungu wa hedhi
Maelezo ya picha,

Ndekela Mazimba anasema kuwa siku hiyo inamsadia kukabiliana na uchungu wa hedhi

Kujadili swala la hedhi hadharani ni knyume na utamaduni wa watu wa taifa la Zambia.

Hii ndio maana kuna sheria za wafanyikazi zinazowaruhusu wanawake walio katika hedhi kuchukua siku moja ya mapumziko inayojulikana 'Mothers day' licha ya kwamba inasimamia wanawake wote iwapo wana watoto au la.

Sheria hiyo haina masharti ,wanawake wanaweza kuchukua siku hiyo kwa matakwa yao wenyewe na sio lazima watoe kithibitisho chochote cha kimatibabu ,hatua inayowalazimu wengine kuhoji kuhusu sheria hiyo.

''Nadhani ni sheria nzuri kwa sababu wanawake hupitia mengi wakati wanapokuwa katika hedhi'', alisema Ndekela Mazimba ambaye anafanya kazi katika idara ya mahusiano ya uma.

Bi Mazimba hajaolewa wala hana watoto lakini huchukua siku yake ya Mothers Day kila mwezi kutokana na uchungu anaopata wakati anapoingia katika hedhi.

''Unaweza kubaini kwamba katika siku yako ya kwanza ya hedhi, unaweza kusikia maumivu mengi katika tumbo.Unaweza kununua dawa zote za kutuliza maumivu lakini unasalia kitandani siku nzima''.

Maelezo ya picha,

Mutinta Musokotwane-Chikopela anasma kuwa tayari Zambia kuna siku nyingi za likizo

''Na mara nyengine, unagundua kwamba watu wengine wanahisi uchungu siku za kwanza za hedhi, lakini siku zinaposonga uchungu unapungua.Mimi hutaka usaidizi siku za kwanza wakati ninahisi uchungu mwingi'',alisema Mazimba

Wanawake nchini Zambia hawalazimiki kufanya maandalizi yoyote kabla ya kupumzika siku hiyo, lakini wanaweza kupiga simu siku hiyo kusema wanachukua Mothers day.

Muajiri anayewanyima wafanyikazi wake siku hiyo anaweza kushtakiwa.

Muajiri wa Bi Mazimba ,Justin Mukosa huunga mkono sheria hiyo na kusema kuwa anaelewa shinikizo wanawake wanayokumbana nayo wanapopima kati ya majukumu ya kifamilia na kazi.

Maelezo ya picha,

Muajiri wa bi Mazimba ,Justin Mukosa anaunga mkono sheria hiyo

Anasema kuwa hatua hiyo inaweza kuwa na athari nzuri kwa kazi za wanawake.

''Utendaji sio tu mtu aliye afisini. Unafaa kupimwa kulingana na uzalishaji wa mtu huyo''.

Lakini anakiri kwamba kuna matatizo katika mfumo huo kutokana na kuwakosa wafanyikazi kupitia notisi fupi mbali na majaribio ya watu kuuchezea.

Unaweza kutumiwa vibaya kwamba pengine mtu ana jambo lake ambalo anataka kufanya kwa hivyo anachukua Mothers day.

Sio kila mtu anaunga mkono siku hiyo ya Mothers Day, na kuna wanawake wengi miongoni mwa wakosoaji.

Mutinta Musokotwane-Chikopela ameolewa na ana watoto watatu.

Anafanya kazi ya ukuzaji lakini hachukui siku ya mothers day akisema kuwa inasababisha uvivu miongoni mwa wafanyikazi wanawake.''Siiamini na siichukui''.

''Hedhi ni jambo la kawaida katika mwili wa mwanamke, ni sawa na kuwa na mimba ama hata kujifungua'',alisema.

Nadhani wanawake huchukua fursa ya siku hiyo hususan kwamba hakuna njia ya kuthibitisha kwamba uko katika hedhi au la. Bi Chikopela anasema kuwa sheria hiyo inafaa kufanywa kuwa wazi zaidi.

''Tatizo la Zambia ni kwamba kuna likizo nyingi sana ,ikiwemo likizo ya siku ya maombi.Kwa hivyo nadhani Mothers day inawafanya wale wanaopenda likizo kufurahi''.

Maelezo ya picha,

Wanawake nchini Zambia ndio wanaohudumia familia zao

Muungano wa vyama vya wafanyikazi nchini zambia ZCTU ,pia inaunga mkono sheria hiyo.

Tumekuwa tukiwaelezea wanawake kwamba inapofikia siku hiyo anafaa kupumzika na hawafai kwenda hata sokoni ama hata kufanya kazi nyengine kwa sababu ni makosa'', alisema Catherine Chinunda katika wakfu wa kitaifa wa ZCTU.

Waziri wa wafanyikazi nchini humo Joyce Nonde-Simukoko ambaye ni mwanaharakati wa zamani wa muungano wa wafanyikazi anahoji kwamba Mothers day ilianzishwa miaka ya 90 kabla ya kufanywa kuwa sheria.

Lakini ana onyo kali kwa mtu yeyote anayetaka kuitumia vibaya sheria hiyo.

''Iwapo unasema kwamba umechukua siku ya Mothers Day halafu upatikane katika densi ,basi haitachukuliwa kama Mothers day.Haufai hata kuonekana mjini ukitengeza nywele zako ama ukinunua vitu sokoni.Unaweza kufutwa kazi.kwa mfano,mtu alipatikana akitekeleza kilimo baada ya kuchukua Mothers day na alifutwa kazi''.