Mpalestina aliyeua wanajeshi Jerusalem aliunga mkono Islamic State

Benjamin Netanyahu Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bw Netanyahu amesema njia zilizotumiwa na mshambuliaji ni sawa na zilizotumiwa Nice na Berlin

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuna dalili kwamba mwanamume aliyevurumisha lori kwenye umati wa watu na kuua wanajeshi wanne Jerusalem alikuwa mfuasi wa kundi linalojiita Islamic State (IS).

Hata hivyo, hajatoa ushahidi wowote kufafanua hilo.

Mwanamume Mpalestina alipigwa risasi na kuuawa.

Mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri kuhusu usalama umeidhinisha kuzuiliwa bila kufunguliwa mashtaka kwa watu wanaoshukiwa kuwa waungaji mkono wa IS.

Mawaziri hao pia wameagiza nyumba ya mshambuliaji huyo ibomolewe haraka iwezekanavyo.

Kundi la Hamas, ambalo linadhibiti ukanda wa Gaza, limesifu shambulio hilo na kulitaja kama hatua ya kupinga hatua ya Israel kuendelea kudhibiti maeneo ya Ukingo wa Magharibi.

Wanawake watatu na mwanamume, wote ambao ni vijana wa miaka 20 hivi, waliuawa kwenye shambulio hilo.

Watu wengine 17 walijeruhiwa, polisi wamesema.

Mshambuliaji ametambuliwa kuwa Fadi Qunbar, 28, kutoka mtaa wa Kipalestina wa Jabel Mukaber mashariki mwa Jerusalem karibu na eneo la shambulio.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jamaa wa Fadi Qunbar akionyesha picha yake kwa wanahabari

Kanda za kamera za CCTV zinaonesha lori likiendeshwa kwa kasi kuelekea walikokuwa wanajeshi hao na kisha kuendeshwa kurudi nyuma kuwaponda.

"Aliendesha lori hilo kurudi nyumba ili kuponda watu zaidi," Leah Schreiber, ambaye alishuhudia shambulio hilo, aliwaambia wanahabari.

"Hilo lilikuwa wazi kabisa."

Jeshi la Israel limesema waliouawa ni Yael Yekutiel, 20; Shir Hajaj, 22; Erez Orbach, 20 na Shira Tzur, 20.

Wanajeshi wengine walimpiga risasi na kumuua Qunbar.

Watu tisa walikamatwa kuhusiana na shambulio hilo, wakiwemo jamaa watano wa mshambuliaji.

Bw Netanyahu alitembelea eneo la shambulio Jumapili alasiri na kusema: "Tunafahamu kwamba kumekuwa na msururu wa mashambulio ya kigaidi.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanajeshi wakumbatiana eneo la shambulio

"Bila shaka, huenda uka uhusiano fulani - kuanzia Ufaransa hadi Berlin, na sasa Jerusalem."

Washambuliaji Nice na Berlin walitumia njia sawa, ya kuvurumisha lori kwenye umati wa watu.

Mkuu wa polisi wa taifa Roni Alseich amesema kuna uwezekano dereva huyo alichochewa na shambulio la mwezi uliopita mjini Berlin.

Kabla ya kisa cha Jumapili, wanajeshi 35 walikuwa wameuawa kwa njia mbalimbali na Wapalestina au Waarabu raia wa Israel tangu Oktoba 2015.

Zaidi ya Wapalestina 200 wameuawa katika kipindi hicho.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii