Hotuba ya Obama: Demokrasia inakuhitaji

Huwezi kusikiliza tena
Obama atokwa na machozi akimshukuru Michelle

Rais wa Marekani Barack Obama amewahimiza Wamarekani kuitetea demokrasia, kwenye hotuba yake ya mwisho kama rais wa Marekani mjini Chicago.

"Kwa kila kipimo, Marekani sasa ni bora zaidi, na ina nguvu zaidi" kuliko ilivyokuwa miaka minane iliyopita alipochukua madaraka, amewaambia maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika mjini humo.

Hata hivyo, "demokrasia inatishiwa kila inapokosa kutiliwa maanani".

Amewaomba Wamarekani wa kila asili kuangazia mambo kutoka kwa msimamo wa wengine, na kusema kwamba "lazima tuwategee sikio wengine na kusikia".

Rais Obama ndiye rais wa kwanza nchini Marekani wa asili ya Afrika na alichaguliwa mwaka 2008 akiahidi kurejesha matumaini na kutekeleza mabadiliko.

Mrithi wake Donald Trump ameahidi kubatilisha baadhi ya sera kuu alizofanikisha Bw Obama, 55.

Bw Trump ataapishwa tarehe 20 Januari.

Umati ulisema kwa sauti "miaka minne zaidi" lakini kiongozi huyo alizipuuzilia mbali.

"Siwezi kufanya hivyo," alisema.

"Marais wa Marekani wanaruhusiwa kuongoza kwa mihula miwili pekee katika katiba."

Bw Obama, aliyeonekana mchangamfu, alisema utamaduni wa kukabidhi madaraka kwa warithi kwa njia ya amani ni moja ya mambo makuu yanayotambuliwa katika demokrasia Marekani.

Lakini amesema kuna mambo matatu yanayotishia demokrasia Marekani - ukosefu wa usawa kiuchumi, mgawanyiko kwa misingi ya rangi na hatua ya baadhi ya makundi kwenye jamii kujitenga na kuwa na misimamo ambayo haiongozwi na ukweli.

Akikamilisha hotuba yake, amesema ombi lake moja la mwisho kabisa kwa Wamarekani akiwa kama rais ni: "Nawaomba muwe na imani. Si katika uwezo wangu wa kuleta mabadiliko - bali katika uwezo wenu."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Obama amesema Makamu wa Rais Joe Biden amekuwa kama ndugu kwake
Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Amewashukuru mke wake Michelle na mabinti wao Malia (pichani) na Sasha kwa kujinyima mambo mengi

Obama alikuwa amerejea Chicago, pahala ambapo alitangaza ushindi mwaka 2008 na kutoa hotuba iliyokuwa sana na ujumbe wa matumaini baada ya kipindi cha kampeni za mgawanyiko kati ya Bw Trump na Bi Hillary Clinton.

Bw Obama alisema Wamarekani wengi wa umri mdogo, wakiwemo wale walioshiriki kampeni zake na wanaoamini katika "Marekani ya usawa, haki na inayojumuisha watu wote" wanampa matumaini zaidi sasa kuliko alivyokuwa alipoanza.

Kwa kuchagua Chicago, Bw Obama alisema awali kwamba alitaka kurejea pahala ambapo "mambo yote yalianzia" kwake na Mkewe Michelle Obama, badala ya kutoa hotuba yake hiyo kutoka White House.

Hotuba hiyo iliandikwa kwa wazo la kuwazungumzia Wamarekani wote, wakiwemo wafuasi wa Trump, maafisa wake walisema.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Bw Obama alihitimisha kwa kusema: "Yes we can. Yes we did. Yes we can." (Ndio Twaweza. Ndio tuliweza. Ndio tunaweza."

Ziara hiyo ya Bw Obama mjini Chicago ndiyo yake ya mwisho kama rais, na safari yake ya 445 akiwa ameabiri ndege ya rais ya Air Force One.

Watu zaidi ya 20,000 walitarajiwa kuhudhuria hotuba hiyo yake katika ukumbi wa mikutano wa McCormick Place, ambao ndio mkubwa zaidi Amerika Kaskazini na ukumbi ambao Bw Obama alitoa hotuba mwaka 2012 baada ya kumshinda Mitt Romney uchaguzi wa 2012.

Tiketi zilitolewa bila malipo lakini kuna watu walikuwa wanaziuza $1,000 (£820) mtandaoni saa chache kabla ya hotuba yake kuanza.

Umekuwa ni utamaduni kwa rais kutoa hotuba ya mwisho Marekani kwa muda mrefu.

Marais wa zamani George W Bush na Bill Clinton walitoa hotuba zao kutoka White House, lakini George Bush Snr alitoa hotuba yake kutoka chuo cha jeshi cha West Point.

Anapoondoka madarakani, Rais Obama anaungwa mkono na 57% ya Wamarekani, kwa mujibu wa kura ya maoni ya Associated Press-NORC Center for Public Affairs Research poll, kiwango sawa na cha Bill Clinton alipokuwa anaachia madaraka.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii