Somalia: Al-Shabab waua walioshiriki mapenzi ya jinsia moja

Wapiganaji wa al-Shabab Haki miliki ya picha AP
Image caption Kundi la al-Shabab lina uhusiano na mtandao wa al-Qaeda

Wanamgambo wa kundi la al-Shabab wamewaua kwa kuwapiga risasi watu watatu kusini mwa Somalia, wawili kati yao kwa makosa ya kushiriki mapenzi ya jinsia moja.

Mwanamume wa tatu aliuawa kwa kufanya ujasusi dhidi ya kundi hilo.

Sheikh Mohamed Abu Abdalla, gavana mwanachama wa al-Shabab alisema Isak Abshirow, 20, na Abdirizak Sheikh Ali, 15, walifumaniwa na wapiganaji wa al-Shabab wakifanya mapenzi.

Wanaaminika kuwa watu wa kwanza kuuawa na al-Shababkwa makosa ya kushiriki mapenzi ya jinsia moja.

Saeed Mohamed Ali alipatikana na kosa la kufanyia ujasusi vikosi vya Ethiopia ambao ni sehemu ya kikosi cha wanajeshi wa Muungano wa Afrika wanaokabiliana na wanamgambo hao.

Wanaume hao waliuawa hadharani na katika mji Buale ambako umati mkubwa wa watu ulikuwa umekusanyika.

Mtandao mmoja ulio na ufungamano na kundi hilo, umeripoti kuwa mahakama ya Kiislamu katika eneo la Jubba iliwapata wanaume hao na hatia.

Kushiriki mapenzi ya jinsia ni hatia kisheria katika mataifa mengi ya Afrika na hukumu yake huwa ni kifungo grezani.

Kupigwa risasi

"Jaji alitoa hukumu ya wanaume hao watatu hadharani na kuwapata na hatia. Walipigwa risasi na kuawa katika mji wa Buale," Sheikh Abdalla, aliliambia shirika la habari la Reuters.

Afisa wa serikali ya Somalia amesema kesi yoyote juu ya mapenzi ya jinsia moja nchini Somalia, taifa lenye idadi kubwa ya waumini wa dini ya Kiislamu, inafaa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sharia.

Hata hivyo hakufafanua jinsi sheria hiyo itakavyotekelezwa.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii