Nigeria kumpa hifadhi rais Yahya Jammeh iwapo atajiuzulu

Rais wa Gambia Yahya Jammeh kupewa hifadhi nchini Nigeria iwapo atakubali kujiuzulu
Image caption Rais wa Gambia Yahya Jammeh kupewa hifadhi nchini Nigeria iwapo atakubali kujiuzulu

Bunge nchini Nigeria limeunga mkono mswada wa kumpatia hifadhi rais Yahya Jammeh iwapo atajiuzulu.

Alipoteza uchaguzi mnamo mwezi Disemba ,lakini anataka matokeo ya kura hiyo kufutiliwa mbali.

Wabunge hao walitumia takriban nusu saa kujadili pendekezo hilo lililowasilishwa na Fani Zoro anayesimamia kamati ya wakimbizi bungeni.

Bunge lilikuwa limefurika ,baada ya wawakilishi hao kutoka katika likizo yao ya mwaka uliopita.

Baadhi ya wanachama hawakuunga mkono mapendekezo hayo wakisema kuwa wanamtambua rais Jammeh kuwa dikteta aliyechukua uongozi kupitia mapinduzi 1994 na kudai kuwa hatua kama hiyo itatuma ujumbe mbaya kwa viongozi wengine.

Hatahivyo wabunge wengi waliunga mkono wakisema itakuwa njia ya kuzuia mgogoro zaidi.

Iwapo ghasia zitaibuka nchini Gambia maafa yake yataathiri eneo lote la magharibi ,walidai.

Wengi wa wafanyikazi wa serikali wanaofanya kazi nchini Gambia ni raia wa Nigeria ,waliongezea.