Barrow amtaka Jammeh kushiriki mazungumzo

Adama Barrow na Yahya Jammeh

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Adama Barrow na Yahya Jammeh

Mshindi wa Uchaguzi wa Rais nchini Gambia Adama Barrow amemtaka Rais anayemaliza muda wake Yahya Jammeh kushiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja ili kutatua mgogoro wa kisiasa ulioikumba nchi hiyo.

Katika Mahojiano na BBC, Barrow amesema anauhakika kwamba ataapishwa kama kiongozi mkuu wa taifa hilo wiki ijayo, licha ya Rais Jammeh kukataa kukubali kushindwa katika uchaguzi huo uliofanyika mwezi uliopita.

Wasuluhishi kutoka Jumuia ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS wanatarajiwa kuwasili Gambia baadaye leo katika jaribio lingine la kumtaka Rais Jammeh kukubali kuondoka madarakani, wakati awamu yako itakapomalizika Jumatano wiki ijayo.

Iwapo atakataa viongozi hao wa ECOWAS wamesema watazingatia kumuondoa kwa nguvu madarakani.

Rais Jammeh amepeleka shauri mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo.