Betri mpya inayoweza kuzima moto yavumbuliwa

Simu Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Betri za lithium-ion ni maarufu sana katika vifaa vya kielektroniki

Wataalamu nchini Marekani wamevumbua betri ya lithium ambayo ina kemikali inayoiwezesha kuzima moto iwapo utazuka kwenye betri.

Kemikali hiyo itafunguliwa iwapo kiwango cha joto kwenye betri kitapanda sana.

Kemikali hiyo ambayo kwa lugha ya kitaalamu hufahamika kama triphenyl phosphate (TPP) itakuwa ndani ya mfuko ambao utakuwa umewekwa ndani ya majimaji ambayo hutumiwa na betri kuhifadhi na kuachilia nguvu za umeme.

Mfuko huo huyeyuka kiwango cha joto kinapofikia nyuzi 150C (302F), na kuachilia kemikali hiyo.

Wakati wa kufanyiwa majaribio, kemikali hiyo iliweza kuzima moto kwa sekunde 0.4 pekee.

Betri za lithium-ion hutumiwa kwenye mitambo na vifaa vingi vya elektroniki lakini huwa hatari kwa moto

Wataalamu wa Chuo Kikuu cha Stanford wametangaza uvumbuzi wao kwenye makala iliyochapishwa kwenye jarida la Science Advances.

Majaribio ya awali ya kuweka kemikali ya TPP ndani ya betri bila kuiweka ndani ya mfuko fulani yalikuwa yanaathiri utendakazi wa betri.

Betri ya lithium-ion inapowekwa chaji haraka au kuwe na kasoro fulani, kunaweza kukatokea mgongano wa nguvu za umeme na kusababisha moto.

Februari 2016, Bodi ya Usalama katika Uchukuzi wa Taifa Marekani ilitoa tahadhari kuhusu kuwekwa kwa betri za lithium kwenye mizigo. Bodi hiyo ilisema betri hizo zinaweza kusababisha moto au mlipuko.

Haki miliki ya picha Ariel Gonzalez
Image caption Simu za Galaxy Note 7 ambayo inadaiwa kushika moto baada ya chaja kuchomolewa

Ingawa Samsung hawajatoa bado matokeo ya uchunguzi wake kuhusu kilichosababisha moto katika simu zake za Galaxy Note 7 ambazo zilishika moto mwaka jana, baadhi ya ripoti zinadokeza kwamba huenda moto ulitokana na kasoro kwenye betri.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii