Mawaziri watatu zaidi wajiuzulu Gambia

Yahya Jammeh Haki miliki ya picha AFP
Image caption Yahya Jammeh

Mawaziri watatu nchini Gambia wamajiuzulu wakati Rais Yahya Jammeh akipuuza wito wa kumtaka aondoke madarakani wakati muhula wake utakapokamilika siku ya Alhamisi.

Mawaziri wa mashauri ya nchi za kigeni, fedha na biashara walijiuzulu kwa mujibu wa mtandao wa Fatu.

Wiki iliyopita waziri wa habari Sheriff Bojang na Alieu Jammeh wa michezo nao walijiuzulu.

Maelfu ya watu wamekuwa wakikimbia kwenda nchi jirani ya Senegal na hadi nchini Guinea-Bissau, kutokana na hofu kuwa huenda kukazuka ghasia, kufuatia hatua ya Rais Jammeh ya kukataa kukubali kushindwa kwenye uchaguzi wa mwezi Disemba.

Mfanyabiashara Adama Barrow ambaye kwa sasa yuko nchini Senegal ameapa kuchukua madaraka.

Barrow alimshinda Yahya Jammeh ambaye aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1994.