Abdilatif Abdalla, mwandishi aliyeonja mateso ya kalamu

Huwezi kusikiliza tena
Abdilatif Abdalla ,mwandishi na mwanaharakati wa siasa

Abdilatif Abdalla mwandishi na mtunzi mzaliwa wa Kenya aishiye Hamburg nchini Ujerumani, alilazimika kuishi nje ya nchi yake kwa miaka zaidi ya 22 tangu miaka ya 1970 mara baada ya kutoka katika gereza ambalo alifungwa kutokana na maandishi yake yaliyokuwa yakiikosoa serikali ya Jomo Kenyatta.

Ni katika kipindi hicho cha kuitumikia adhabu yake gerezani, ndipo alipoandika kazi zaidi za uandishi kwa siri .

Mwandishi wa BBC Arnold Kayanda alizungumza na Abdilatif alipokuwa mjini Dar es salaam kushiriki katika tukio la utoaji Tuzo kwa washindi wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika.

Image caption Abdilatif Abdalla,Mwanaharakati na mwandishi wa lugha ya kiswahili

Abdilatif Abdalla ni mwandishi na mwanaharakati wa siasa aliyefungwa kutokana na kukiunga mkono chama cha upinzani cha Kenya People's Union kilichoanzishwa kuwatetea wananchi wakati wa utawala wa rais wa wakati huo Jomo Kenyatta mwaka 1969-1972.

Ilikuwa ahukumiwe kunyongwa iwapo asingejitetea na kushinda shitaka la kwanza la uhaini, lakini shitaka la uchochezi hakuweza kulikwepa.

Abdilatif Abdalla alizaliwa Mombasa Kenya mnamo mwaka 1946 ambako alilelewa na babu yake Mzee Ahmad Basheikh Bin Hussein ambaye ndiye hasa aliyepanda mbegu ya uandishi wa mashairi kwa mjukuu wake.

Ni kazi yake iliyoitwa Kenya Twendapi iliyosababisha kutiwa nguvuni katika kipindi ambacho serikali haikupendezwa na harakati za chama cha KPU.

Abdilatif Abdalla, kwanza alifungwa katika Gereza la Kaliti na kisha kuhamishiwa Shimo la Tewa.

Ilikuwa katika muda huo wa kufungwa kwake alipoandika Shairi lake maarufu la Sauti ya Dhiki.

Baadaye alihamia Tanzania ambako alianza kufundisha na kutafiti Lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kisha alihamia London ambako alifanya kazi katika Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC kabla ya kuhamia Ujerumani ambako alifundisha Kiswahili kwa miaka mingi katika Chuo Kikuu cha Leipzig.