Madonna akana madai ya kupanga watoto kutoka Malawi

Madonna ameshapanga watoto wawili kutoka Malawi Haki miliki ya picha AP
Image caption Madonna ameshapanga watoto wawili kutoka Malawi

Mwanamuzizi nyota wa Pop Madonna, amekana madai kuwa ametuma maombi ya kupanga watoto wawili zaidi kutoka nchini Malawi.

Hii ni baada ya msemaji wa serikali ya Malawi kuviambia vyombo vya habari kuwa mwanamuziki huyo wa umri wa miaka 58, alikuwa amefika mahakamani kuweka ombi la kutaka kupanga watoto.

Madonna ambaye kwa sasa yuko nchini Malawi amesema kuwa ziara yake ni kihisani.

"Uvumi kuhusu kupanga watoto si ukweli," alisema Madona.

"Niko Malawi kuangalia hospitali ya watoto mjini Blantyre na kazi nyingine ndio nielekee nyumbani.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Madonna (mwenye miwani) akiwa na watoto, kutoka kushoto , David, Lourdes, Mercy na Rocco

Awali Madonna alikuwa amechukua watoto wawili wa kupanga kutoka nchini Malawi, David Banda mwaka 2006 na Mercy James mwaka 2009.

Uhusiano wa nyota huyo na Malawi ulianza mwaka 2006, wakati alibuni shirika lenye lengo la kuboresha maisha ya watoto.

Pia alikuwa na mpango wa kujenga shule ya wasichana, kwa gharama ya dola milioni 15, lakini badala yake akabadili mawazo na kutumia fedha hizo kufadhili shule kadha.

Madonna ana watoto wawili Lourdes na Rocco kutoka uhusiano wa awali. Mwaka uliopita alikabiliwa na kesi kuhusu Rocco na mumewe wa zamani Guy Ritchie.

Alishindwa katika kesi hiyo na Rocco akahamia London kuishi na babake.