Katibu wa Joseph Goebbels afariki dunia akiwa na miaka 106

Brunhilde Pomsel, Juni 29, 2016. Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Bi Pomsel alikubali tu kuzungumzia maisha yake baadaye kabisa maishani

Brunhilde Pomsel, katibu wa zamani wa mkuu wa propaganda wa watawala wa Nazi nchini Ujerumani Joseph Goebbels, amefariki dunia akiwa na miaka 106.

Kazi yake ilimfanya kuwa na uhusiano wa karibu na Goebbels - mmoja wa wahalifu wabaya zaidi wa kivita wa karne ya 20.

Alikuwa mmoja wa wafanyakazi wakuu wa chache wa Nazi ambao bado walikuwa hai.

Alikubali kuzungumza kuhusu aliyopitia wakati wa utawala wa Nazi mwisho mwisho wakati wa uhai wake.

kwenye makala ya video iliyoandaliwa hivi majuzi, alisema hakufahamu lolote kuhusu mauaji ya Wayahudi milioni sita.

Kwenye makala hiyo iliyopewa jina "A German Life" (Maisha ya Kijerumani), ambayo ilizinduliwa mwaka jana, alisema hana majuto yoyote - "ila tu iwao mtalaumu Wajerumani wote" (kwa makosa yaliyotekelezwa na watawala wa Nazi).

Bi Pomsel alizaliwa Januari 1911 na alifanya kazi kama mwandishi wa wakala wa bima wa Kiyahudi kwa miaka kadha kabla ya kuhama na kuanza kufanya kazi sawa, mara hii kwa mwandishi wa mrengo wa kulia.

Ingawa alikiri kwamba hajawahi kuwa na msimamo wowote kisiasa, alijiunga na chama cha Nazi kilipongia madarakani mwaka 1933 ili kupata kazi ya serikali katika redio ya taifa ya Ujerumani.

Ujuzi wake kama mpiga chapa, anasema, ulimuwezesha kupata kazi ya kuwa katibu wa Joseph Goebbels mwaka 1942, wakati wa vita, Goebbels wakati huo akiwa waziri wa "uhamasishaji wa umma na propaganda".

Haki miliki ya picha Fox Photos / Getty
Image caption Goebbels alikuwa mkuu wa uenezaji propaganda wakati wa utawala wa Nazi

Alimweleza Goebbels kama "mwanamume mtanashati...ingawa mfupi kiasi", ambaye alivalia nadhifu - lakini alikuwa mkali.

Alisema kwamba yeye alikuwa tu katibu wa Goebbels na hakufahamu kuhusu vitendo vya kikatili vilivyotekelezwa na watawala wa Nazi.

"Siwezi kujihisi mwenye lawama. Labda, ufike kiwango cha kulaumu Wajerumani wote kwa kusaidia serikali (ya Nazi) kuchukua udhibiti. Hapo tulishiriki sote Mimi nikiwemo."

Haki miliki ya picha Blackbox Film / A German Life
Image caption Rafiki Myahudi wa Pomsel alifariki akiwa Auschwitz, yeye alipokuwa anamfanyia kazi Goebbels

Rafiki yake Myahudi, Eva Lowenthal, alitoweka Novemba 1943.

Miaka sita baadaye, Bi Pomsel aligundua kwamba alifariki akiwa katika kambi iliyotumiwa kuwafanyisha kazi kwa lazima na kuwaua Wayahudi ya Auschwitz.

Bi Pomsel alikamatwa na majeshi ya Muungano wa Usovieti wakati wa kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Alikaa miaka mitano kizuizini kabla ya kujiunga tena na shirika la utangazaji la Ujerumani mwaka 1950 na kufanya kazi kwa miaka mingine 20.

Hakutamka kuhusu maisha yake na maafisa wakuu wa Nazi hadi mwaka 2011 wakati wa mahojiano na gazeti moja.

Alizungumza tena kwa kina wakati wa kuandaliwa kwa makala ya maisha yake iliyozinduliwa mwaka 2016.

Amefariki dunia akiwa Munich, wiki chache kabla ya kusherehekea miaka 106 tangu kuzaliwa kwake.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii