Aiba dhahabu na kuzificha katika tupu ya nyuma Canada

Leston Lawrence alidaiwa kuiba dola 127,116 za vipande 22 vya dhahabu. Haki miliki ya picha Royal Canadian Mint
Image caption Leston Lawrence alidaiwa kuiba dola 127,116 za vipande 22 vya dhahabu.

Mfanyikazi wa zamani wa kampuni ya Royal Mint nchini Canada amepewa hukumu ya miezi 30 jela kwa kuiba sarafu za dhahabu na kuzificha katika tupu yake ya nyuma.

Leston Lawrence alidaiwa kuiba dola 127,116 za vipande 22 vya dhahabu.

Jamaa huyo mwenye umri wa miaka 35 ambaye alipatikana na hatia mwezi Novemba alipatikana baada ya kufanikiwa kuuza vipande 17 vya dhahabu kupitia kampuni ya wananuzi wa dhahabu wa Ottawa Guld Buyers.

Jaji wa mahakama ya Ontario Peter Doody alimuagiza Lawrence kulipa faini ya dola 145,900.

Akitoa hukumu hiyo siku ya Alhamisi ,alisema kwamba Lawrence anafaa kuhudumia kifungo chengine cha mwezi mmoja jela iwapo atashindwa kulipa faini hiyo baada ya miaka mitatu ya kuachiliwa kwake.

Wachunguzi walipata mafuta ya Vaseline na glovu katika eneo lake la kuweka vitu vyake katika kampuni ya Mint.

Haki miliki ya picha NORMAN MADDEAUX
Image caption Kampuni ya Royal Mint Canada

Jaji Doody amesema kuwa vitu hivyo vilitumika kuwezesha kuingiza dhahabu hizo katika mjiko wake kulingana na ripoti za gazeti la Toronto.

Vipande hivyo 17 vilikuwa na uzani wa gramu 264 na viliuzwa kwa dola 7,300 kila moja kati ya mwaka 2014 na 2015.

Lawrence alipatikana na hatia ya kuiba dhahabu katika kampuni ya Mint na hivyobasi kwenda kinyume na uaminifu aliokuwa amepewa na kampuni hiyo kama mfanyikazi.

Alitumia fedha alizopata kununua boti mjini Florida na kujenga nyumba nchini Jamaica, mahakama iliambiwa.

Kazi ya Lawrence ilikuwa kusafisha dhahabu na mara kwa mara alifanya kazi pekee katika eneo ambalo halikuwa na kamera za usalama.

Alifanya kazi katika kampuni hiyo kutoka 2008 hadi 2015.