Mihadarati: Polisi 12 wasimamishwa kazi Tanzania

Inspekta jenerali wa polisi nchini Tanzania Ernest Mangu
Maelezo ya picha,

Inspekta jenerali wa polisi nchini Tanzania Ernest Mangu

Kikosi cha polisi nchini Tanzania kimewasimamisha kazi kwa muda maafisa 12 wa polisi ambao ni miongoni mwa wale waliotajwa na kamishna wa polisi wa jimbo la Dar es Salaam bw Paul Makonda miongoni mwa watu wanaoshirikishwa na ulanguzi wa mihadatari .

Pia amesema kuwa uchunguzi unaendelea dhidi ya idadi kubwa ya wasanii ambao pia walitajwa na Makonda na kuripoti katika vituo vya polisi ili kuhojiwa.

Kulingana na Gazeti la The Citizen nchini humo Inspekkta Jenerali Ernest Mangu amesema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya maafisa hao 12 uchunguzi utakapokamilika.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam Simon Sirro amesema operesheni ya kuwakamata watu hao ilianza tangu jana ambapo watu watano walitiwa korokoroni na kufikisha idadi ya watu waliokamatwa hadi leo kufikia 17.

Maelezo ya sauti,

Wasanii, polisi mbaroni kwa tuhuma za mihadarati Tanzania

Kamanda Sirro amesema kwa sasa imeundwa timu maalum inayowahusisha polisi na vyombo vingine vya usalamaya ili kuendelea kuwatafuta wafanya biashara wa madawa hayo.

Biashara ya madawa ya kulevya ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili nchi ya Tanzania ambapo baadhi wamekuwa wakiinyooshea kidole serikali kwamba hajaichukua hatua kali ya kukabiliana na tatizo hilo.