Ziara ya matibabu ya rais Buhari yawatia wasiwasi raia Nigeria

Rais Buhari wa Nigeria
Image caption Rais Buhari wa Nigeria

Kushindwa kwa rais Buhari wa Nigeria kubaini muda anaotaka kuongezewa ili kuendelea na likizo yake ya matibabu mjini London inawatia wasiwasi raia wa taifa hilo.

Kumekuwa na uvumi kuhusu afya ya rais huyo tangu alipoondoka nchini humo wiki mbili zilizopita.

Alimkabidhi rasmi makamu wake wa rais majukumu yake Prof Yemi Osinbajo hatua inayoungwa mkono na baadhi ya wataalam kama ishara ya heshima kwa katiba na sheria ya taifa hilo.

Licha ya kwamba mambo yanaendelea kama kawaida tangu rais Buhari aondoke, kutokuwepo kwake huenda kusikubalike na baadhi ya raia kutokana na hali mbaya ya uchumi wa taifa hilo unaozidi kuzorota.

Likizo hiyo ya kimatibabu pia imeshutumiwa na wataalam wa afya ambao wanasema kuwa rais huyo angesalia nyumbani na kupewa matibabu.

Huwezi kusikiliza tena
Buhari: Mke wangu kwake ni jikoni

Muungano wa maafisa wa matibabu nchini Nigeria ulikasirishwa na ziara kama hiyo nchini Uingereza mwaka uliopita ili kutibiwa sikio lake ukisema taifa hilo lina madaktari bingwa ambao wangemtibu.

Waziri wa afya Daktari Osagie Ehanire anasema kuwa Nigeria hutumia zaidi ya dola bilioni moja kila mwaka kwa ziara za kimatibabu kitu ambacho serikali ya sasa iliahidi kupunguza.

Haijajulikana ni matibabu hayo yatamgharimu pesa ngapi bw Buhari na ni nani atakayegharimika.

Lakini kama raia nambari moja nchini humo, serikali inatarajiwa kugharamikia matibabu yake.

Hatahivyo, raia wengi wa Nigeria hawatakuwa na raha kugundua kwamba ni ziara ngapi kama hizo zitalipokonya taifa hilo mapato ya kigeni.