Askari Nigeria, wampiga mlemavu

Haki miliki ya picha @GALACTICOHD/TWITTER
Image caption Mtu huyu anaonekana kurushwa kutoka kwenye kiti chake cha magurudumu

Askari wawili nchini Nigeria wamekamatwa na kuhukumiwa kwa kosa la kumpiga mtu mmoja mlemavu, baada ya kunaswa katika video, wakimpiga kwa fimbo mtu huyo katika barabara moja yenye shughuli nyingi.

Jeshi linasema kuwa sababu ya kichapo hicho kwenye mji wa Onitsha ulioko katika jimbo la Anambra Jumanne wiki hii, inasemekana alikuwa amevalia shati lilokuwa na madoa doa kama la jeshi.

Taarifa inaongeza kuwa wanajeshi hao wamehukumiwa "kutokana na hatua zetu za kutokubalia kabisa utovu wa nidhamu".

Raia wengi nchini Nigerian, wamekuwa wakilalamika kuwa wanajeshi wengi huwa hawaadhibiwi kwa kutumia nguvu kupita kiasi.

Makundi ya kutetea haki za binadamu mara kwa mara yamekuwa yakilaumu jeshi la Nigeria kwa mateso dhidi ya raia, hasa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, ambapo limekuwwa kikikabiliana na kundi la wanamgambo wa Boko Haram.

Kuvalia mavazi yalio na mabaka mabaka kama magwanda ya kijeshi ni swal tete nchini Nigeria, kwa sababu wanamgambo na wahalifu mara nyingi hujificha kwa kuvalia mavazi hao na kisha kutekeleza mashambulio au kujifanya ni maafisa wa polisi ili kutekeleza uhalifu.

Kifungu cha sheria nambari 110 cha uhalifu nchini Nigeria, kinasema kuwa ni uvunjaji wa sheria ya Nigeria kwa kuvalia magwanda ya kijeshi au mavazi "yanayofanana na nguo za jeshi".

Mkanda huo wa video kuhusu kisa hicho kilichotendeka kusini mwa Nigeria, umesambazwa sana katika mtandao wa kijamii kabla ya Jeshi kutoa taarifa.

Jeshi lilisema "ni kitendo kibaya mno" kilikuwa "kisa ambacho hakijawahi kufanyika na wala hakionyeshi ukweli halisi wa jeshi la Nigeria".

Taarifa ya kuhukumiwa kwa wanajeshi hao wawili, inatukia wiki moja tu baada ya mwanajeshi mmoja alihukumiwa jela miaka 7, kwa kumpiga risasi na kumuuwa raia katika soko moja mjini Maiduguri, kaskazini mashariki mwwa Nigeria mwaka uliopita.

Askari huyo hakutajwa, lakini alipatikana na hatia ya muwaji.