Jaji aamrisha Rais wa zamani wa Peru Alejandro Toledo, kukamatwa

Alejandro Toledo alikuwa Rais wa Peru kati ya mwaka 2001 hadi 2006 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Alejandro Toledo alikuwa Rais wa Peru kati ya mwaka 2001 hadi 2006

Jaji mmoja nchini Peru ameamrisha kukamatwa kwa rais wa zamani wa nchi hiyo Alejandro Toledo.

Bw Toledo, aliyeongoza Peru kuanzia mwaka 2001 hadi 2006, anatuhumiwa kupokea hongo kutoka kwa kampuni moja ya ujenzi ya Brazil, Odebrecht ili ipewe kandarasi ya ujenzi chini ya wizara ya wafanyikazi.

Rais huyo kwa sasa hayuko nchini Peru bali yuko Paris Ufaransa, lakini makao yake ni Marekani.

Katika mahojiano ya hivi majuzi ya Runinga, alikanusha kufanya lolote baya.

Jaji Richard Concepcion aliamuru kuwa Bw Toledo anafaa kukamatwa na kuzuiliwa korokoroni haraka iwezekanavyo, huku akikataa katu ombi la mawakili wa Rais huyo wa zamani wa kupewa dhamana.

Kampuni ya Odebrecht imejipata katika kashfa kubwa ya ufisadi ya kutoweka kwa mabilioni ya pesa.

Katika sehemu ya makubaliano yake na maafisa wa sheria wa Marekani, kampuni hiyo imekubali kwamba ililipa karibu dola milioni 800 kama mlungula kwa serikali za mataifa ya Amerika Kusini.

Walikiri kulipa dola milioni 29 nchini Peru ili kupewa kandarasi hiyo kati ya mwaka 2005 na 2014.

Waliendelea kufanya hivyo hata wakati wa utawala wa Bw Toledo na warithi wake wawili Alan Garcia na Ollanta Humala.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wapeelelezi wakiisaka nyumba ya Bw Toledo mjini Lima, Jumamosi

Warithi wake hao pia wamekanusha kufanya lolote baya.

Vyombo vya habari nchini Peru vinaripoti kuwa, afisa mkuu mtendaji wa zamani wa kampuni ya Odebrecht nchini Peru, Jorge Barata, anamtuhumu Bw Toledo kwa kupokea dola milioni 20 kama hongo ili kumpuni hiyo ipewe kandarasi ya kujenga barabara kuu inayounganisha Peru na Brazil.

Bw Barata anashirikiana na waendesha mashtaka katika taifa alimozaliwa Brazil na taifa la Peru kama sehemu ya kutaka kusamehewa.

Kupinga madai

Bw Toledo amepinga vikali madai hayo na kusema: "Namtaka Bw Barata aseme, ni lini, wakati upi, kwa njia gani na ni benki ipi alituma dola hizo milioni 20. Sitavumilia hili!"

Jumamosi iliyopita, wapelelezi walipekua nyumba ya Bw Toledo kwa masaa matano.

Mwanasheria mkuu anasema kuwa stakabadhi zilizopatikana nyumbani kwake zitapigwa msasa.

Wakati wa msako huo Bw Toledo alikuwa amesafiri Ufaransa huku akisema kuwa "nimetamaushwa mno na uteketezaji huu wa kisiasa kutoka kwa maadui wangu wa jadi".

Rais wa sasa wa Peru, Pedro Pablo Kuczynski, amesemai kuwa Bw Toledo anafaa kurejea Peru ili kujibu maswali mengi dhidi yake.