Mkalimani aliyetafsiri visivyo matamshi ya mtalii afikishwa mahakamani Tanzania

Simon Sirikwa alitafsiri visivyo matamshi ya mtalii
Image caption Simon Sirikwa alitafsiri visivyo matamshi ya mtalii

Mkalimani mmoja nchini Tanzania, ambaye alikamatwa kwa kutoa kanda ya video ambayo alikuwa akitafsiri visivyo matamshi ya mtalii, amefikishwa mahakamani leo.

Mkalimani huyo alikamatwa wiki iliyopita kufuatia agizo la wizara ya utalii. Simon Sirikwa alifikishwa katika mahakama ya Musoma Kaskazini Magharibu mwa Tanzania kwa kile mamlaka zinasema kuwa kuichafulia jina nchi.

Akiongea na BBC kamanda wa eneo la Mara Jaffer Mohammed, anasema kuwa uchunguzi umeonyesha kuwa kanda ya Video ya Simon, inakiuka sheria ya uhalifu wa mitandao.

Alikamatwa siku ya Ijumaa kwenye mpaka kati ya Serengeti na Arusha, ambapo amekuwa akifanya kazi kama mwelekezi wa watalii kwa karibu miaka 10.

Kabla akamatwe, Sirikwa alirekodi video nyingine ambapo anaoneka akiwa na mtalii ambaye hakutajwa jina, akiomba msamaha kwa vitendo vyake.

Bwana Sirikwa ambaye kwa jina la utani anafahamika kama Pondamali, amerekodi video kadha za vichekesho ambazo anachapisha katika ukurasa wake wa Facebook.