Mume mzinifu ashtaki Uber nchini Ufaransa

Alitumia simu ya mkewe ambayo iliendelea kupokea ujumbe na hivyo mke akaanza kumshuku mumewe Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mwanamme huyo aliomba huduma ya Uber na kufunga kaunti, lakini Uber haikufunga

Mfanyabiashara mmoja kusini mwa Ufaransa ameishtaki kampuni ya huduma ya Teksi ya 'Uber' Ufaransa, baada ya mkewe kufahamu kwamba safari zake alizofanya na magari hayo zilikua kumtembelea mpenzi wake.

Kwa mujibu wa wakili wake, mwanamme huyo aliitisha huduma ya Uber akitumia simu ya mkewe.

Licha ya mwanamme yule kufunga akaunti alioomba huduma ile, upande wa Uber haukufunga bali uliendelea kutuma jumbe kwa simu ya mkewe kuhusu safari yake na hii ilimfanya mke yule kuanza kumshuku mumewe.

Wawili hao wamesha talakiana kutokana na kisa hicho.

Mume aliyeachwa ameshtaki Uber akitaka kulipwa dola milioni 48.

"Mteja wangu amekua muathiriwa na utumizi mbaya wa simu za kampuni", amesema Wakili wake, baada ya kuwasilisha kesi mahakamani.

Wakili anaendelea kusema kasoro za simu zimemsababishia mteja wake matatizo ya ndoa.

Wakili huyo hata hivyo ameongeza kwamba mteja wake hajasema kima anachotaka kulipwa na madai ya dola milioni 48 zilikua taarifa za vyombo vya habari ambazo hazina msingi.

Gazeti moja la Le Figaro limenadi kwamba kumekua na matatizo ya simu za Uber ambapo ukisha funga kaunti yako baada ya kutumia mtandao wake, kampuni hiyo haifungi akaunti hiyo. Uber haijatoa taarifa yeyote kuhusu kisa hiki ila imesema inatilia maanani sana masuala binafsi ya wateja wake.