Nduguye Kim Jong-un auawa nchini Malaysia

Kim Jong-nam hutumia muda wake mwingi nje ya Korea Kaskazini Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kim Jong-nam hutumia muda wake mwingi nje ya Korea Kaskazini

Ndugu wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, ameuawa nchini Malaysia, kwa mujibu wa Korea Kusini.

Kim Jong-nam mwenye umri wa miaka 45, anaripotiwa kulengwa kwenye uwanja wa ndege wa Kuala Lumpur.

Polisi nchini Malaysia wamethibitisha kwa shirika la Reuters kuwa mwanamume raia wa Korea Kaskazini ambaye alifariki wakati akipelekwa hospitalini kutoka uwanja wa ndege ni Bwana Kim.

Kwa mujibu wa ripoti ya televisheni ya Chosum nchini Korea Kusini, Bwana Kim aliwekewa sumu akiwa uwanja wa ndege na wanawake wawili wanaoaminiwa kuwa maajenti wa Korea Kaskazini.

Mwaka 2001 bwana Kim alikamatwa akijaribu kuingia Japan akitumua pasipoti bandia. Aliwaambia maafisa kuwa alikuwa na mpango wa kuzuru eneo la burudani la Disneyland mjini Tokyo.

Kim alikwa akionekana kama mtu ambaye angemrithi babake lakini kitendo hicho kilisababisha wao kutofautiana.

Kim Jong-nam ndiye mtoto wa kwanza wa kiume wa Kim Jong-il, ambaye aliitawala Korea Kaskazini kuanzia mwaka 1994 hadi wakati wa kifo chake mwaka 2011.

Baada ya nduguye mdogo wa kambo kuchukua uongozi wa Korea Kaskazini wakati babake alifariki mwaka 2011, Kim Jong-nam hakuoneka saana na alitumia muda wake mwingi nje ya nchi hasa Macau , Singapore na China.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kim Jong-nam ni ndugu wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un

Alinukuliwa na vyombo vya habari vya Japan akisema kuwa alipinga uongozi wa kupokezana.

Pia alinukuliwa na kitabu kimoja mwaka 2012 akisema kuwa nduguye wa kambo hakuwa na tajriba wa kuongoza.

Bwana Kim amekuwa akilengwa ili auawe siku za hapo nyuma. Jasusi mmoja raia wa Korea Kaskazini ambaye alifungwa nchini Korea Kusini mwaka 2012, aliripotiwa kukiri kuwa alikuwa akipanga njama ya kumuua Kim Jong-nam.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii