Tuzo ya Komla Dumor 2017: Kumtafuta mwandishi nyota wa Afrika

Komla Dumor alifariki ghafla mwaka 2014 akiwa na miaka 41
Image caption Komla Dumor alifariki ghafla mwaka 2014 akiwa na miaka 41

Shirika la Utangazaji la BBC limezindua kampeni ya kumtafuta atakayekuwa mwandishi nyota wa masuala ya Afrika.

Waandishi kutoka Afrika wanaalikwa kutuma maombi yao kupata tuzo ya Komla Dumor. Tuzo hii inanuia kutambua na kukuza vipaji vya uandishi Afrika.

Tuzo hii ilizinduliwa mara ya kwanza mwaka 2015 kwa heshima ya marehemu Komla Dumor mwandishi wa habari wa BBC na mzaliwa wa Ghana aliyefariki dunia ghafla akiwa na miaka 41 mwaka wa 2014.

Itamuendelea mtu ambae anafanya kazi barani Afrika na anaonyesha ujuzi na maadili ya uandishi katika utangazaji na pia ana ustadi wa kuelezea taarifa kutoka Afrika.

  • Ili kufahamu iwapo umehitimu na pia kuwasilisha maombi, bofya hapa

Pia awe na ari ya kuwa mwandishi nyota siku zijazo.

Mshindi atapata nafasi ya kufanya kazi katika afisi kuu za BBC jijini London ambapo atapokea mafunzo na kupewa maarifa zaidi.

Pia atapata nafasi ya kuzuru Afrika kuangazia taarifa fulani, na kisha taarifa yake itatumika kote barani Afrika na dunia.

Nancy Kacungira mtangazaji wa zamani wa runinga ya KTN nchini Kenya alikuwa mshindi wa kwanza mwaka wa 2015.

Didi Akinyelure mwandishi wa habari kutoka Nigeria na ambaye alianza kama mwekezaji wa hisa akashinda mwaka wa 2016.

Image caption Didi Akinyelure alishinda tuzo hiyo mwaka 2016

Wakati wa mafunzo yake, Didi alikwenda nchini Ivory Coast kuangazia nafasi za kampuni za nyumbani katika sekta ya kakao inayotengeneza Chocolate.

Kwa sasa yuko mjini Blantyre Malawi kuzindua tuzo ya mwaka huu 2017 pamoja na Francesca Unsworth ambaye ni mkurugenzi mkuu wa BBC.

"Maisha yangu yamebadilika sana," amesema Didi.

"Daima watu watanifahamu kama mshindi wa tuzo ya Komla Dumor, hii ni hadhi kubwa sana. Unapata mafunzo ya uandishi ikiwemo utangazaji, uhariri na kuandika pamoja na jinsi ya kueleza taarifa yako na kuelewa maadili ya BBC ".

"Huenda una kipaji ambacho BBC inatafuta kwako, hivyo weka manaani nafasi hii na kutuma maombi yako".

Francesca amesisitiza kwamba BBC imejitolea kuendeleza ndoto yake Komla, kwa kusema, "Tumeshatuza na kuwapokea washindi wawili ambao ni waandishi wa hadhi ya juu. Walipata nafasi ya kupata mafunzo nasi na kutoa taarifa zao kutoka Afrika kwa wafuasi wetu wa BBC. Najivunia sana kukutana na kuwafahamu Nancy na Didi. Pia tumejifunza mengi kutoka kwa washindi wetu hasa jinsi ya kuwaelewa wafuasi wetu. Tunatumaini kumpata mwandishi mwingine nyota wa Afrika na kumpokea kama mshindi mpya wa Tuzo ya Komla Dumor".

Maombi yote yatachunguzwa kwa makini na wana jopo wenye ustadi akiwemo; Rachel Akidi kutoka makala ya 'BBC Focus on Africa', Paul Royall ambae ni mhariri wa runinga ya 'BBC UK TV' ambayo hutayarisha taarifa kuu ya habari ya saa kumi na mbili na saa nne usiku.

Pia yuko Khadijah Patel ambae ni mhariri wa gazeti la Mail & Guardian la Afrika Kusini.

Khadija amefurahia sana kuwa mwana jopo na amesema, "Kazi ya Komla ilitugusa wengi wetu. Waliomfahamu walimpenda sana, zaidi aliheshimiwa na wengi. Kazi yake ilikuwa ushuhuda wa nguvu ya waandishi wa habari wa Afrika. Ninafurahia sana kuwa mmoja wa kuheshimu ndoto yake".

Wanaotuma maombi wana hadi saa 23.59GMT Machi 15 mwaka huu 2017 kuwasilisha maombi yao.

  • Kwa taarifa zaidi kuhusu masharti na jinsi ya kutuma maombi tembeleabbc.com/KomlaDumor
  • Ili kufahamu iwapo umehitimu na pia kuwasilisha maombi, bofya hapa
  • Pia unaweza kutumia kitambulisha mada #BBCKomlaAward kwenye Twitter kuwajulisha wengi kuhusu tuzo hii.