Robert Harward akataa kazi ya Trump kuwa mshauri wa usalama wa taifa

Robert Harward Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Robert Harward, 60, ni mwanajeshi wa zamani wa jeshi la majini la Marekani

Mwanajeshi wa zamani aliyekuwa amependekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump kuwa mshauri wake wa masuala ya usalama wa taifa amekataa kazi hiyo.

Robert Harward alitarajiwa na wengi kuchukua wadhifa huo ulioachwa na Michael Flynn aliyefutwa kazi na Bw Trump Jumatatu.

Afisa mmoja wa ikulu ya White House alisema sababu ya Bw Harward kukataa nafasi hizo ni kwamba ana majukumu mengi ya kifamilia na kifedha.

Bw Flynn alimpotosha makamu wa rais Mike Pence kuhusu mazungumzo yake na balozi wa Urusi nchini Marekani ambayo aliyafanya kabla yake kuteuliwa rasmi kuwa mashauri.

Pigo hilo kwa Bw Trump, la kukataliwa kwa uteuzi wake na Harward, lilitokea saa chache baada ya Bw Trump kupuuzilia mbali ripoti kwamba utawala wake umekumbwa na mtafaruku mkubwa.

Alisisitiza kwamba utawala wake unafanya kazi kama "mashine iliyoundwa vyema."

Bw Harward aliambia shirika la habari la Associated Press kwamba utawala wa Trump ulikubali sana kuzingatia "mahitaji yangu, ya kitaalamu na kibinafsi".

"Ni suala la kibinafsi tu," alisema Harward, 60, ambaye kwa sasa anafanya kazi Abu Dhabi kama afisa mkuu mtendaji wa kampuni inayofanyia kazi jeshi la Marekani ya Lockheed Martin.

Alipoulizwa kuhusu taarifa kwamba alikuwa amewasilisha ombi la kutaka aruhusiwe kuhama na wafanyakazi wake binafsi serikalini, Bw Harward alisema: "Nafikiri rais ndiye anayefaa kuzungumzia hilo."

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption David Petraeus (kushoto) na Keith Kellogg ni baadhi ya wanapigiwa upatu kuchukua wadhifa huo

Watu wawili wanaopigiwa upatu sana kupewa wadhifa huo ni Jenerali mstaafu David Petraeus na kaimu mshauri mkuu wa masuala ya usalama wa taifa Keith Kellogg.

Bw Kellogg, ambaye ni jenerali mstaafu wenye nyota tatu, aliteuliwa kuhudumu kama kaimu baada ya Bw Flynn kung'atuka.

Ana miaka 72 na amehudumu kwa muda mrefu jeshini, ambapo alipigana vita Vietnam na Iraq kabla ya kustaafu 2003 na kuwa mshauri wa masuala ya usalama wa kampuni ya programu za kompyuta ya Oracle Corp.

Bw Petraeus, ni jenerali wa zamani mwenye nyota nne, ambaye alistaafu kama mkuu wa CIA mwaka 2012 baada ya kubainika kwamba alikabidhi nyaraka zenye siri kuu kwa mwandishi aliyekuwa akiandika kitabu kuhusu maisha yake, ambaye alikuwa ameingia kwenye uhusiano nje ya ndoa naye.

Bado anatumikia adhabu ya kuwa chini ya uangalizi kwa miaka miwili kwa kosa la kutomakinika akiwa na nyaraka za siri.

Atahitajika kumfahamisha afisa wa jela anayemfuatilia iwapo atahitaji kuhamia Washington DC.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii