Miss Tanzania aliyejitolea kukabili ukeketaji wa wasichana

Huwezi kusikiliza tena
Miss.Tanzania apambana na ukeketaji nchini Tanzania

Miss Tanzania, Diana Edward ameingia katika tasnia ya urembo nchini Tanzania akiwa na malengo tofauti kabisa wakati anashikilia taji lake la urembo kwa mwaka 2016/2017.

Diana Edward ambaye ametoka katika jamii ya Kimaasai anaamini kuwa urembo ni zaidi ya muonekano wa mavazi mazuri, kupamba uso kwa podana kuvaa wigi, ila urembo ni kuwa na malengo, kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Na ameamua kutumia urembo wake kwa kuanza kusaidia jamii yake kutokomeza mila potovu ya ukeketaji kupitia kampeni yake ijulikanayo kama "Dondosha Wembe".

Ametoka katika moja ya makabila ambayo yameathirika zaidi na ukeketaji kwa wasichana nchini Tanzania.

Diana anasema alipata wazo la kuanzisha kampeni ya dondosha wembe kwa kuwa yeye mwenyewe ameponea chupuchupu kufanyiwa kitendo hicho cha ukeketaji baada ya kwenda kupata elimu mbali kidogo na nyumbani kwao, lakini angeweza kuwa miongoni mwa waathirika wa ukeketaji.

Image caption Diana anatoka jamii ya Wamaasai ambayo ni miongoni mwa zilizoathiriwa zaidi

Hivyo jambo hilo lilimfanya afikirie sana na kuanza kutafuta msaada kidogo wa kusaidia jamii yake kwa kuwa anaona waathirika wakubwa wa vitendo vya ukeketaji ni wasichana wenye umri sawa na wake.

"Nashukuru Mungu kwa kuwa nimeweza kupata kidogo ambacho kinaniwezesha kufikia baadhi ya jamii zinazoathirika na ukeketaji na kuwapa elimu juu ya athari za mila na desturi hiyo," anasema.

Diana Edward ana umri miaka 18 na anatoka famila ya watoto wanne, yeye akiwa mtoto wa tatu,

"Dondosha wembe" ni neno linalomaanisha kuwa ni muda sasa wa kudondosha kile kiwembe kinachotumika na mangariba kukeketa na kuachana na mila potovu ya ukeketaji.

Miss Tanzania aliyejitolea kukabili ukeketaji Diana ameanza kufanikisha malengo yake hayo kwa kuanzia kwenye jamii yake ya Kimaasai huku akiwa na malengo ya kueneza kampeni hiyo nchi nzima.

Kwa sasa amebuni njia mbalimbali za kuwafikia walengwa kwa kusafiri kutoka mjini mpaka walipo huko vijijini, mkoa wa Arusha na akifika katika maeneo yao huwa njia anayotumia ni kutengeneza urafiki nao kwa kuishi maisha yao kuanzia mavazi, kuwa na nywele za asili, kula chakula pamoja nao na kuwaonesha kuwa yeye ni mtoto wao.

Shughuli yote huchukua siku tatu au nne, ili aweze kujitambulisha na kutengeneza urafiki na wanakijiji wahusika na hata kupeleka zawadi ndogo ndogo kwao kama pipi kwa watoto, kuwaonyesha picha na kuzungumza nao kwa upendo.

Image caption Diana hulazimika kukumbatia mavazi na vyakula vya jamii yake anapofika vijijini

Ikiwa kubadili mila na desturi za jamii fulani sio jambo rahisi hivyo Diana hujaribu kutafuta watu wa kumsaidia kwanza kwa kupata ruhusa kutoka kwa viongozi wa vijiji ili kuweza kuwafikishia ujumbe wake kwa kufuata desturi na sheria zao, kuhudhuria sherehe zao na kuongea na wazee katika tafrija zao.

Katika kuendesha kampeni hiyo, Diana huongea na wasichana wa umri wake na kupata fursa ya kutoa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji kwa watoto wa shule za msingi.

Kwa kuwa anaamini kama mtoto wa darasa la pili au tatu akijua athari za ukeketaji ana uwezo wa kujiokoa katika ukeketaji kwa kuwa atajua madhara ya suala hili, na hata akiona mzazi anataka kumfanyia kitendo hicho basi ana uwezo wa kukimbia na kutoa taarifa hata kwa mwalimu wake.

Diana, anatoa elimu pia kwa wanaume, kwa kuwa anadhani kwamba wanaume watapata ufahamu juu ya athari za ukeketaji, wataachana na vigezo vya kuhitaji kuoa wanawake ambao wamekeketwa hivyo hata mangariba ambao wao ni wanawake wanaofanya shughuli hiyo watakosa soko kwa kuwa huhitaji wa wanawake ambao wamekeketwa utapungua au kuisha kabisa.

Ingawa matumaini yake ni kufika Tanzania nzima ila bado uwezo wake mdogo kwa kuwa bado anahitaji msaada wa watanzania wenyewe,wanasaikolojia ,madaktari na polisi.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii