Mshukiwa wa mauaji ya Kim Jong nam akamatwa

Kim Jong nam Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kim Jong nam

Polisi wa Malaysia wamesema kuwa wamemtia mbaroni mwanamume mmoja kutoka Korea Kaskazini kuhusiana na mauaji ya Kim-Jong-nam - kaka wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un.

Maafisa wa uchunguzi wanasema kuwa mtu huyo ni wa nne kutiwa mbaroni kuhusiana na mauaji hayo.

Mtu huyo ametajwa kama Ri Jong Choi.

Huyu ni mshukiwa wa kwanza raia wa Korea kutiwa mbaroni na maafisa wa polisi wa Malaysia tangu mauaji ya Kim Jong-nam mnamo Jumatatu.

Maafisa wa Serikali wanasema kuwa ana umri wa miaka 46 na alitiwa mbaroni katika eneo la Kuala Lumpur.

Mmoja wa wanawake aliyetiwa mbaroni awali aliambia polisi kuwa alidanganywa kushiriki katika mauaji hayo akidhania kuwa ulikuwa mchezo wa utani katika kituo cha televisheni.

Sababu maalumu ya kuuawa kwa Bwana Kim hakujulikani.

Matokeo ya uchunguzi wa kifo chake hayajatolewa na kuna uvumi kuwa huenda uchunguzi wa pili ukafanywa.

Maafisa wa Serikali wa Malaysia wamekataa ombi la Korea Kaskazini kuwa maiti yake itolewe upesi ipelekwe nchini humo.