Majina wa wapenzi wa jinsia moja kuchapishwa Tanzania

Wapenzi wa jinsia moja
Image caption Wapenzi wa jinsia moja

Naibu waziri wa afya wa Tanzania, Hamis Kigwangalla ameendelea kusisitiza azma yake ya kuchapisha orodha ya majina ya watu anaowashutumu kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja

Katika mjadala mkali ulioendelea kwenye mtandao wa twitter na watumiaji wengine, Kigwangalla ametetea uamuzi wake huo kwa kusema watu hawa si tu wanajihusisha na vitendo visivyokubalika katika jamii. bali pia wanauza ngono kwa njia ya mtandao na kuhamasisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja vyote vikiwa kinyume na sheria za nchi

"Kuna watu wanadhani vita dhidi ya ushoga ni ya mzaha, ni vita kubwa na tutaishinda. Mtandao ni mrefu na nitaendesha operation kamata kamata," aliandika Kigwangala katika Twitter wiki iliyopita

Lakini mwisho wa wiki katika majibishano yake na watumiaji wengine wa Twitter, Kigwangala ambaye taaluma yake ni Utabibu, alidai kwamba ushoga si swala la kibaolojia lakini ni utashi wa mtu na kwamba ni aina tu ya maisha ambayo watu wa mjini wamechagua kujihusisha kwayo.

Aliendelea kwa kutoa mfano kwamba katika vijiji vya mji anaotoka Nzega, katikati Magharibi mwa Tanzania, hakuna kabisa vitendo vya ushoga.

Wengi katika twitter walimshutumu Kigwangalla kwa kuendesha kampeni ya chuki dhidi ya kundi hilo la mashoga huku yeye akijibu, "natimiza wajibu wangu kama kiongozi msimamizi wa sheria na sera za nchi yetu."

Hatua hii ya Kigwangalla inaambatana na uamuzi wa serikali kuvifungia vituo vipatavyo 40 vya afya ambavyo vilikuwa vikitoa huduma za UKIMWI ikiwa ni pamoja na kwa makundi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsi moja

Nchini Tanzania, mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria na adhabu yake inaweza kuwa hata miaka 30 jela.