Watanzania waendelea kuikimbia Msumbiji

Watanzania

Chanzo cha picha, JERRY MICHAEL

Maelezo ya picha,

Wengi wamefika kituo cha mpakani cha Kilambo

Mamia ya Watanzania waliokuwa wakiishi Msumbiji wanaendelea kuondoka nchini humo kurudi nyumbani Tanzania.

Wengi wamefika katika ofisi ya Uhamiaji ya Tanzania mpakani eneo liitwalo Kilambo wakitaka kurejea.

Magari ya jeshi pia yameanza kusaidia kuwachukua kutoka mpakani na kuwasambaza mikoani kule wanakotokea.

Wiki iliyopita, takriban raia 132 wa Tanzania waliokua wanaishi nchini Msumbiji walitimuliwa nchini humo huku wengine ambao idadi yao haikujulikana wakidaiwa kukamatwa kufuatia operesheni ilioanzishwa na serikali ya taifa hilo.

Chanzo cha picha, JERRY MICHAEL

Kulingana na serikali ya Msumbiji operesheni hiyo ililenga kuwatimua raia wa kigeni wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki nchini Tanzania ilisema kuwa raia waliofukuzwa ama hata kukamatwa ni wale walioishi mji wa Monte Puez kwa kuwa una raia wengi wa kigeni ikilinganishwa na miji mingine.

Chanzo cha picha, JERRY MICHAEL

Kulingana na taarifa hiyo ya serikali ya Tanzania, tayari ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji unaendelea kufanya mawasiliano ya kidiplomasia na serikali ya Msumbiji ili kuwahakikishia usalama raia wa Tanzania na mali yao nchini humo.