"Kasisi" aliyemuua albino ashtakiwa Afrika Kusini

Bhekukufa Gumede alidaiwa kuwalipa wanaume watatu kumuua Thandazile Mpunzi mwezi Agosti mwaka 2015

Chanzo cha picha, TWITTER/ TIMES LIVE

Maelezo ya picha,

Bhekukufa Gumede alidaiwa kuwalipa wanaume watatu kumuua Thandazile Mpunzi mwezi Agosti mwaka 2015

Gazeti la Times Live nchini Afrika Kusini limeandika taarifa ya kutisha kusuhu kushtakiwa kwa mganga moja wa kienyeji ambaye anatuhumiwa kumuua mwanamke moja mwenye ulemavu wa ngozi au albino.

Bhekukufa Gumede, alidaiwa kuwalipa wanaume watatu kumuua Thandazile Mpunzi mwezi Agosti mwaka 2015, kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani.

Mganga huyo alikuwa akihitaji viungo vya mwanamke huyo ili atengeneze dawa ya kienyeji, kwa mujibu wa gazeti hilo.

Mahakama iliambiwa kuwa Gumede aliwashauri wanaume hao kuweka peni kwenye kinywa cha mwanamke huyo kisha watamke maneno fulani ili kumshinda nguvu.

Gumede mwenye umri wa miaka 67, pia anafahamika kama kasisi ambaye anaongoza kanisa la New Star Church in Zion, lenye matawi 15 kote nchini.