Polisi Tanzania wazuiwa kumkamata Mbowe

Mbowe

Chanzo cha picha, ChademaMedia / Twitter

Maelezo ya picha,

Polisi wamezuiwa kumkamata Mbowe hadi Ijumaa

Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam imewaamuru maafisa wa polisi kutomkamata Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe, hadi Ijumaa.

Bw Mbowe alikuwa amefika katika mahakama hiyo kufuatilia mwenendo wa kesi ya kikatiba aliyoifungua dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Camilius Wambura.

Katika kesi hiyo, mbali na mambo mengine, Mbowe anapinga amri ya Makonda ya kutaka akamatwe na pia kile alichokiita kudhalilisha watu wakati mkuu huyo wa mkoa alipotaja majina ya watu wanaodaiwa kuhusika katika ulanguzi na matumizi ya dawa za kulevya.

Kesi hiyo iliahirishwa mpaka saa saba mchana ambapo walipoingia mahakamani kwa mara nyingine, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliamuru Jeshi la Polisi kumkamata Freeman Mbowe hadi Februari 23 maombi yake yatakaposikilizwa.

Mahakama imeambia jeshi la polisi kwamba linaweza kumuita Freeman Mbowe kwa mahojiano kama litaona umuhimu wa kufanya hivyo, lakini hawaruhusiwi kumkamata.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayepingwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho, amefika mahakamani kusikiliza mwenendo wa mgogoro baina yake na Maalim Seif Sharif Hamad ambapo baada ya kumalizika kwa kipindi cha mahakama, alipata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama Kuu ya Tanzania, Lipumba alisema anaunga mkono suala la watuhumiwa wa dawa za kulevya, kukamatwa na kuongeza kuwa serikali inapaswa kuungwa mkono katika suala hilo.

Lakini Lipumba aliongeza kuwa, serikali isikurupuke kuwapeleka watu mahakamani bila kuwa na ushahidi wa kutosha kwani suala hilo litaigharimu fedha nyingi katika kuendesha kesi hizo.