Watu 3.8m wajiandikisha kupiga kura Kenya

Wafula Chebukati
Maelezo ya picha,

Tume ya IEBC imeanza kuwasajli Wakenya wanaoishi nchi wanachama wa EAC na Afrika Kusini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Kenya (IEBC) imetangaza kwamba ilifanikiwa kuwasajili wapiga kura 3.8 milioni katika kipindi cha mwezi mmoja wa kuwasajili kwa wingi wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika mwezi Agosti.

Idadi hiyo ni asilimia 62 ya jumla ya wapiga kura 6 milioni ambao tume hiyo ililenga kuwasajili katika kipindi hicho.

Shughuli ya kuwasajili kwa wingi wapiga kura ilitarajiwa kumalizika Februari 14 lakini mahakama ikaongeza muda wa siku tano hadi Jumapili Februari 19.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati ameambia wanahabari kaunti iliyoongoza kwa idadi kubwa ya wapiga kura kujitokeza kati ya waliolengwa ni Kajiado, kusini mashariki mwa Kenya, ambapo asilimia 240 walijitokeza.

Kaunti ya Mandera kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ilifuata kwa asilimia 116 kujitokeza.

Kwa jumla ya idadi ya wapiga kura waliojitokeza, jiji la Nairobi linaongoza kwa wapiga kura 461,346 likifuatwa na kaunti ya Kiambu (225,995) na jimbo la Nakuru likawa la tatu na wapiga kura 175,756.

Bw Wabukati amesema tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2013, idadi ya wapiga kura waliojitokeza sasa imefikia 5.2 milioni.

Maelezo ya picha,

Baadhi ya wanaume wakisajiliwa kama wapiga kura nchini Kenya kufuatia kuanzishwa kwa shughuli hiyo siku ya Jumatatu

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, wapiga kura 1 milioni waliwasilisha maombi ya kubadilisha vituo vyao vya kupigia.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IEBC Marjan Hussein Marjan ameambia BBC kwamba suala la kuchukua kura na kuipiga huwa ni hiari na kwamba hatua ya watu kutojiandikisha ilivyotarajiwa siyo sababu raia hawana imani na taasisi yake.

Kwa sasa tume hii inatarajia kuanza kuwasajili raia wa Kenya wanaoishi katika mataifa ya Afrika Mashariki, sambamba na katika magereza kote nchini Kenya.

Nje ya nchi, usajili unafanyika Dar es Salaam, Arusha, Kampala, Kigali, Bujumbura na Pretoria.

Macho yote sasa yanaelekea katika mchujo wa vyama vya kisiasa ambapo kumezuka mjadala wa kitaifa hususan baada ya chama tawala Jubilee kuomba tume hiyo kusimamisha mchujo huo. Katiba inakubalia tume kusimamia shughuli hiyo, lakini wasi wasi wa sasa ni ikiwa hali hii huenda ikaweka dosari uhuru wa tume ya uchaguzi.

Aidha tume hii inakumbwa na changamoto ya kuanza kandarasi mpya ya kuchapisha makaratasi ya kura baada ya mahakama moja nchini Nairobi kubatilisha kandarasi iluiyotolewa hapo awali.

Mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati amesema IEBC imeanza utaratibu wa kutoa kandarasi na kwamba tume yake itakua tayari kuendesha uchaguzi huru na haki.