Aliyekatwa mikono kwa utasa sasa ni mjamzito

Jackline Mwende alikatwa mikono na mumewe

Chanzo cha picha, EVANS HABIL/NATION MEDIA GROUP

Maelezo ya picha,

Jackline Mwende alikatwa mikono na mumewe

Mwanamke ambaye alishambuliwa na mmewe na kukatwa mikono nchini Kenya, baada ya ndoa yao kuvunjika kwa kishindwa kuzaa mtoto, sasa anaripotiwa kuwa mjamzito.

Muda mfupi baada ya kushambuliwa, Jackline Mwende alisema kuwa madaktari walikuwa wamewajulisha kuwa yeye alikuwa na uwezo wa kushika mimba, lakini mmewe Stephen Ngila, hakuwa na uwezo wa kuzaa.

Kwenye mahojiano na gazeti na Daily Nation, Mwende amesema kuwa hali hii ilichangia aanze uhusiano mwingine.

Anasema alikuwa na haja ya kuwa na watoto ndipo akaanza uhusiano na mwanamume mwingine ili kuokoa ndoa yake, lakini mumewe ambaye sasa anakabiliwa na kesi ya kutaka kuua akagundua.

"Nilikuwa ninataka mtoto. Nilikuwa na haja ya mtoto...na pia ibilisi alisababisha mimi kutembea nje ya ndoa yangu. Haikuwa vizuri kufanya hivyo, ninajua watu watanihukumu vikali kwa sababu ya hilo. Kwa vile niko hai na nitajifungua mtoto hivi karibuni, nini matumaini licha ya kupitia taabu." Alisema mwende.