Upinzani wasaini makubaliano ya kuungana Kenya

Viongozi wa upinzani nchini Kenya Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Musalia Mudavadi
Maelezo ya picha,

Viongozi wa upinzani nchini Kenya Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Musalia Mudavadi

Viongozi wa muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya NASA wamesaini makubaliano ya kugawana mamlaka ambayo yatawaunganisha dhidi ya chama tawala Jubilee katika uchaguzi mkuu ujao.

Makubaliano hayo yanashirikisha mapendekezo ya kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri mkuu ambao kulingana na duru za chama hicho utamwendea mgombea atakayeibuka wa tatu katika mchujo uteuzi wa mgombea wa urais.

Duru katika mkutano huo zinasema mgombea atakayeshinda uteuzi huo atapeperusha bendera ya chama hicho huku mgombea atakayeibuka katika nafasi ya pili akichukua wadihfa wa naibu wa rais.

Makubaliano hayo ya viongozi wakuu wa NASA, waliokutana kuyaangazia siku ya Jumatano kufuatia madai kwamba yalikuwa tayari yamefichuliwa, pia yanamtaka rais atakayechaguliwa kutumia uwezo wake kubuni wadhifa wa Waziri Kiranja.

Muungano huo baadaye utafanya mabadiliko ya kikatiba ili kubadilisha afisi ya waziri huyo kuwa ile ya waziri mkuu kama ilivyokuwa katika serikali ya muungano ya 2008-2013.

Viongozi wakuu wa muungano huo ni waziri mkuu wa zamani Raila Odinga {ODM}, makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka{WDM}, wazri wa zamani wa mambo ya nje Moses Wetangula{FKenya } na naibu waziri mkuu wa zamani Musalia Mudavadi{ANC}.

Nyadhifa nyingine ambazo viongozi hao wanatumia ili kusalia pamoja ni Spika wa seneti, Kiongozi wa wengi katika bunge la seneti na kiongozi wa wengi katika bunge la uwakilishi.