Peter Maina, Kijana Mkenya anayeunda kiti cha magurudumu cha kipekee

Bw Maina
Maelezo ya picha,

Bw Maina

Katika eneo la Ongata Rongai, viungani mwa jiji la Nairobi, ukiingia katika chumba cha Peter Maina, unaweza kudhani umeingia katika karakana katika chuo kikuu au chuo cha kiufundi.

Kuna vifaa na mitambo ambayo hujawahi kuiona kwingine - utaona kigari ambacho kinadhibitiwa kwa kompyuta, kicheza muziki kinachojitanua, helikopta mfano ambayo inaweza kupaa, na pia kiti cha magurudumu ambacho kinaweza kupanda vidato.

Kuna pia vipande vya plastiki, vyuma na nyaya, vyote ambavyo yeye huvitumia katika ubunifu wake.

Bw Maina, 26, alianza kufanyia majaribio ustadi wake wa kuunda vitu mbalimbali akiwa bado mdogo.

Akiwa na umri wa miaka 7, baada ya wazazi wake kukosa fedha za kumnunulia vitu vya kuchezea, alijiundia basi ndogo kwa kutumia mabati na mashine ya mota. Basi hilo lilikuwa na uwezo wa kujiendesha na hapo ndipo ari ya kubuni vitu tofauti ilipoanzia, anasema.

Maelezo ya picha,

Kicheza muziki

Maelezo ya video,

Kijana mvumbuzi wa mitambo Kenya

Alipomaliza shule ya msingi, Maina hakufikisha alama zilizohitajika za kujiunga na chuo kikuu kutimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi.

Alitumia miezi sita, usiku na mchana, kutengeneza kigari ambacho kina gia 90 na ambacho linauwezo wa kufungua na kujifunga sehemu mbalimbali.

Kijana huyo alitumia kigari hicho kudhihirisha uwezo wake na mwishowe akajipata nafasi ya kujiunga na chuo cha mafunzo anuwai baada ya kukataliwa na vyuo vingi nchini Kenya.

Baada ya kupata mafunzo ya ufundi wa mitambo, aliamua kutengeneza kigari cha magurudumu hususan kwa mwalimu wake Wairimu ambaye alikuwa akiugua ugonjwa wa mifupa uliomlazimisha mwalimu huyo kuacha kufunza.

Ilikuwa vigumu kwa mwalimu wake huyo kupanda na kushuka ngazi au vidato na hata kuandika ubaoni.

Maelezo ya picha,

Maina alianza kuunda kigari cha magurudumu kumsaidia mwalimu wake

Maina alitumia muda wa miezi sita kuchora mchoro wa kigari hicho na miaka miwili kuunganisha sehemu tofauti za kigari hicho.

"Nilitumia muda mrefu kwa sababu nilihitaji kufanya utafiti kuhusiana na mahitaji ya watu wenye ulemavu wa kutembea na pia nilikuwa na tatizo kubwa la fedha," anasema Bw Maina.

''Baada ya muda, mwalimu wangu alifariki bila kujua nilichokuwa namtengenezea, ilinisikitisha sana. Baadaye, niliamua kutengeneza kifaa cha muziki kwa sababu mimi mwenyewe napenda muziki."

Chombo hicho kinafahamika kama 'Music DNA' ambacho kina uwezo wa kutoa marangi tofauti zaidi ya 90 kwa nusu saa kulingana na mdundo wa muziki.

Chombo hicho kinatumia komputa ndogo kukiwezesha kufanya kazi.

Amebuni pia kigari kidogo cha futi moja nukta tano ambacho hutumia kitenza mbali (remote).

Maelezo ya picha,

Kicheza muziki

Kigari hicho ni hususan kwa kubebea kamera kwa wapenzi wa kupiga picha katika mbuga za wanyama, ambapo mhusika hawezi kuwakaribia wanyama mwitu kupata picha kwa karibu. Alibuni kigagari hicho baada ya kupata changamoto kutoka kwa rafiki yake ambaye hupenda kupiga picha .

Kwa hivi sasa Maina ameamua kuwashirikisha wenzake kutengeneza kiti halisi cha magurudumu ambacho kitakuwa na uwezo wa kuwasaidia watu wenye ulemavu wa kutembea kufika maeneo mengi ambayo hayafikiki kwa urahisi, mfano majumba ya ghorofa.

Anatarajia kwamba kitakapokamilika, kitakuwa kimemgharimu dola 4,000 za Marekani.