Burundi yasema UN inapendelea upinzani nchini humo

Burundi inataka mshauri wa UN katika mazungumzo hayo Benomar Jamal kuondolewa kwa madai ya kupendelea upinzani
Maelezo ya picha,

Burundi inataka mshauri wa UN katika mazungumzo hayo Benomar Jamal kuondolewa kwa madai ya kupendelea upinzani

Umoja wa mataifa umetoa wito kwa pande zinazokinzana katika mgogoro wa kisiasa nchini Burundi kujitolea kwa dhati katika kutafuta suluhu la mgogoro huo.

Umoja huo unasema serikali ya Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza imekataa kushiriki majadiliano ya sasa kuhusu swala hilo huko Tanzania.

Katika ripoti kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa katibu mkuu wa umoja huo , Antonio Guterres, amesema wakati umefika kwa wadau wote kuweka tofauti zao kando na kujali maslahi ya taifa lao kuliko maslahi yao binafsi.

Serikali ya Burundi kwa upande wake inadai Umoja huo unawapendelea wapinzani wao na kutaka mshauri mmoja wa ngazi ya juu katika Umoja wa Mataifa anaehusika na swala hilo Benomar Jamal aondolewe kutoka mazungumzo hayo.

Mzozo wa sasa wa Burundi uliripuka pale rais Pierre Nkurunziza alipowania na kushinda muhula wa tatu uongozini katika uchaguzi uliokumbwa na utata tele.