Tanzania kuimarisha biashara na Uganda

Rais Museveni wa Uganda na mwenzake wa Tanzania John Pombe Magufuli

Chanzo cha picha, Ikulu ya Tanzania

Maelezo ya picha,

Rais Museveni wa Uganda na mwenzake wa Tanzania John Pombe Magufuli

Serikali ya Tanzania imesema kuwa itaimarisha biashara yake na Uganda kwa lengo la kuinua uchumi wa raia wa mataifa hayo mawili.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema kuwa tayari Tanzania imeanza kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) ambayo itakwenda pamoja na ujenzi wa bandari kavu Mkoani Mwanza ili kuwapunguzia muda wa usafiri wafanyabiashara wa Uganda wanaolazimika kusafiri hadi bandari ya Dar es Salaam kuchukua mizigo yao inayotoka nje ya nchi kwa meli.

Aidha amesema kuwa serikali yake itakarabati meli ya MV Umoja itakayovusha mizigo hadi bandari ya Port Bell kupitia ziwa Viktoria, mbali na kununua ndege 6 za kusafirisha kwa ajili ya Shirika la ndege la Taifa (ATCL) na kupunguza vizuizi vya barabarani hadi kufikia 3.

"Uwekezaji wa wafanyabiashara wa Uganda hapa nchini Tanzania una thamani ya dola za Marekani milioni 46.05 na umezalisha ajira 1,447"

"Watanzania wanaoishi Uganda ni wengi kuliko wanaoishi katika nchi nyingine yoyote duniani, hii ina maana tunapaswa kushirikiana zaidi na kufanya biashara zaidi"

Kuhusu mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania, Rais Magufuli amesema Tanzania ipo tayari kuanzisha ujenzi huo baada ya kukamilisha mazungumzo ya masuala machache yaliyokuwa yaliosalia na ametaka wawekezaji waanze kazi badala kutoa visingizio.

Kwa upande wake Rais Museveni amemshukuru Rais Magufuli kwa mapokezi mazuri aliyoyapata akisema Uganda itaendelea kuwa ndugu na rafiki wa kweli wa Tanzania huku akisisitiza kuwa rafiki na ndugu wa kweli ni lazima wawe wamoja katika maamuzi na mipango mbalimbali ikiwemo maendeleo na biashara.

Vilevile Rais Museveni ametoa wito kwa nchi za Afrika Mashariki na Afrika nzima kuzungumza lugha moja na kuwa na msimamo wa pamoja ili kukabiliana na ukoloni ambao huko nyuma ulitawala kutokana na watawala wa Afrika kukosa umoja.

Kuhusu bomba la Mafuta, Rais Museveni amesema atafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo hasa baada ya uamuzi kufanyika kuwa bomba la mafuta yaliyogundulika Hoima nchini Uganda litapitia Tanzania hadi bandari ya Tanga.