Maelfu wakusanyika kumkumbuka Nemtsov Urusi

Boris Nemtsov alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Vladimir Putin
Maelezo ya picha,

Boris Nemtsov alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Vladimir Putin

Melfu ya wafuasi wa kiongozi wa upinzani aliyeuwawa nchini Urusi, Boris Nemtsov, wanafanya mhadhara kukumbuka siku aliyouwawa miaka miwili iliyopita.

Wanasiasa kadha wa upinzani wanatarajiwa kushiriki katika maandamano, pamoja na mwanasiasa mashuhuri kabisa anayemlaumu Rais Putin, Alexei Na-valny.

Mihadhara pia inatarajiwa kufanywa katika miji ya St Petersburg na Yekaterinburg.

Bwana Nemtsov, aliyewahi kuwa naibu waziri mkuu, aliuwawa alipokuwa akipanga kuchapisha nyaraka, kuonyesha jinsi Urusi ilivyohusika katika mashariki mwa Ukraine.

Wanaume watano kutoka Chechenya walifanyiwa kesi mwezi wa Oktoba, kwa mauaji ya mawanasiasa huyo.

Naye mwanaharakati maarufu wa upinzani nchini Urusi, Ildar Dadin, amefunguliwa kutoka gereza lililo mbali, kusini mwa nchi.

Maelezo ya picha,

Ildar Dadin aliachiliwa kutoka gerezani leo Jumapili

Amefunguliwa baada ya mahakama kuu kufuta kesi yake awali juma hili.

Baada ya kuachiliwa huru Bwana Dadin alilakiwa na mkewe na wafuasi, na aliviambia vyombo vya habari, kwamba ataendelea kupinga aliyoita, serikali ya kifashisti ya Vladimir Putin.

Alifungwa kwa kufanya maandamano ya amani mara kadha dhidi ya Rais Putin, na kutetea wafungwa wa kisiasa.

Maelezo ya picha,

Mwili wa Nemtsov ukiwa kwenye daraja la Moskvoretsky baada ya kuawa