Morocco kujitoa eneo la Guerguerat

Morocco
Image caption Mfalme Mohamed VI wa Morocco

Morocco imesema itajitoa katika eneo lenye mgogoro la Magharibi mwa Sahara ambalo liliibua hali ya wasiwasi na Polisario Front ambao walijitenga.

Wizara ya mambo ya nje mjini Rabat, imesema itaendelea na zoezi la kujitoa kutoka eneo hilo maarufu kama Guerguerat.

Wizara imesema uamuzi huo umechukuliwa na mfalme Mohamed VI kufuatia ombi la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Mfalme alimpigia bwana Guterres siku ya Ijumaa, akiutaka Umoja wa Mataifa kuchukua hatua ili kusitisha kile alichokiita uchokozi wa Polisario.

Morocco inasisitiza kwamba Magharibi mwa Sahara ni sehemu ya eneo lake, lakini Polisario inaitisha kura ya maoni ya uhuru.