Mourinho amtaka Ibrahimovic kuongeza kandarasi

Mshambuliaji wa manchester United Zlatan Ibrahimovic Haki miliki ya picha EPA
Image caption Mshambuliaji wa manchester United Zlatan Ibrahimovic

Mkufunzi wa klabu ya Manchester United Jose Mourinho anamtaka mshambuliaji wa klabu hiyo Zlatan Ibrahimovic kusalia katika klabu hiyo kwa mwaka mwengine mmoja.

Ibrahimovic mwenye umri wa miaka 35 alijiunga na Manchester United akiwa mchezaji huru kutoka Paris-St Germain kwa kipindi cha msimu mmoja huku akiwa na nafasi ya kuongeza kandarasi yake.

Raia huyo wa Sweden amefunga magoli 26 katika mechi 38 msimu huu,zikiwemo bao mbili katika ushindi wa kombe la EFL dhidi ya Southampton.

''Sote tunataka asalie na tunaamini atafanya hivyo kwa msimu mwengine mmoja'', alisema mkufunzi huyo.

Ibrahimovic alibeba kombe lake la 32 katika kipindi chake chote cha soka baada ya kufunga bao la dakika 87 katika uwanja wa Wembley .

Katika kipindi hicho Manolo Gabiadiani aliifungia Saints mabao mawili baada ya Jesse Lingard kuiweka Red Devils ikiwa inaongoza kwa 2-0.

Mourinho aliongezea: Sipendelei kum'bembeleza mchezaji kutia saini kandarasi mpya ama kunichezea.Wakati Zlatan alipoelekea Barcelona kutoka Inter Milan nilihisi vibaya sana.Lakini iwapo anahitajika mashabiki wanaweza kwenda hadi mlangoni kwake kupiga kambi usiku kucha.