Serikali ya Kenya kuondoa matangazo magazeti ya kibinafsi

Baadhi ya magazeti ya kibinafsi nchini Kenya
Maelezo ya picha,

Baadhi ya magazeti ya kibinafsi nchini Kenya

Serikali ya Kenya imetangaza kuwa itasitisha matangazo yake kupitia magazeti ya kibinafsi nchini humo, katika hatua ambayo ina lengo la kupunguza matumizi.

Serikali inasema kuwa hutumia karibu dola milioni 20 kwa matangazo ya magazeti katika masuala kama zabuni za serikali, nafasi za ajira na matangazo mengine ya umma.

Ilani ya serikali imeyashauri mashirika ya serikali kutoa matangazo yao kupitia jarida mpya la serikali la My.Gov.

Wakati wa kikao maalum cha mawaziri tarehe 8 mwezi Februari, baraza hilo liliidhinisha kubuniwa kwa gazeti ambalo litasambazwa kwa wingi ambalo litaitwa MY.GOV, ambalo litaelezea kwa kina sera za serikali.

Ikiwa hatua hiyo itaidhinishwa, itasababisha hasara kubwa na watu wengi kupoteza kazi katika sekta ya uandishi wa habari.

Gazeti la Nation linaripoti kuwa magazeti ya The Star na The People Daily, yamefikia makubaliano na serikali kusambaza gazeti hilo la serikali kwa malipo.